***********************
Na Englibert Kayombo, WAMJW – Arusha
Wataalam wa Afya nchi wametakiwa kuchukua vipimo kwa washukiwa wa ugonjwa wa corona na sii kuangalia kwenye tatizo la upumuaji pekee.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel alipokuwa ziara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru kujionea hali ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa corona.
“Tunakubali kuwa ugonjwa upo lakini tunawataka wataalam wetu wa afya kufanya vipimo zaidi na kujiridhisha kuwa ni ugonjwa wa corona au ni matatizo tuu ya kawaida ya upumuaji” amesema Dkt. Mollel
Ametolea mfano wa Hospitali ya Mount Meru ambayo hadi leo ilikuwa na washukiwa 44 wa ugonjwa corona huku wagonjwa waliopimwa na kuthibitishwa kuwa na ugonjwa wa corona walikuwa ni 4.
Aidha Dkt. Mollel amesema kuwa hali ya ugonjwa huo inasimamiwa vizuri na wataalam wa afya nchini huku akiwatoa hofu wananchi kuwa idadi ya wagonjwa hao waliopo nchini kuwa sii kubwa.
“Licha ya kuwa na idadi ndogo ya wagonjwa wa corona haimaanishi tusiendelee kuchukua hatua hapana, sasa wimbi la tatu la ugonjwa wa corona hapa nchini, tuendelee kuchukua tahadhari zote zinazotolewa na wataalam wetu, tuzingatie kunawa mikono mara kwa mara, kuvaa barakoa pamoja na kuepuka mikusanyiko” amesisitiza Dkt. Mollel
“Tuendelee kufanya yote kwa namna ya kujikinga toka kwenye wimbi la kwanza, la pili na sasa tuko kwenye wimbi la tatu, zile taratibu zote ambazo zimetufanya sisi tupite salama kipindi kile nazo tuendelee kufanya zikiwemo kula matunda pamoja na kutumia tiba asili katika kujikinga dhidi ya ugonjwa huu” amefafanua zaidi Dkt. Godwin Mollel
Dkt. Mollel amesema kuwa katika wimbi hili la tatu kirusi cha ugonjwa wa corona kimekuwa kikali na tofauti kama ilivyokuwa katika wimbi la kwanza na pili kupelekea Wizara kuja na mkakati mpya wa kutoa elimu zaidi juu ugonjwa huo pamoja na kupita kwenye hospitali kujionea hali halisi ya ugonjwa wa corona kwenye vituo hivyo vya kutolea huduma za afya nchini.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bi. Vones Uisso amemshukuru Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel kutembelea Mkoa wa Arusha hususani Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Bi. Uisso amesema kuwa Uongozi wa Mkoa umejipanga kuendelea kutoa elimu kwa umma na kuwatahadharisha wananchi kufuata maelekezo yote yanayotolewa na viongozi pamoja na wataalam wa afya.
Amesema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa imepanga kufanya kikao cha pamoja na viongozi wote kuanzia ngazi ya kijiji mpaka mkoani kuweka mikakati endelevu ya uhamasishaji wananchi juu ya kujikinga na ugonjwa wa corona.