Baadhi ya Wafanyabiashara wa Soko la Jumbi Wakizungumza na Waandishi wa habari kuhusu kuomba kurejeshwa mnada wa Nazi katika Soko la Jumbi Wilaya ya Magharibi “B”.
Picha na Maryam Kidiko / Maelezo Zanzibar.
***********************
Na Kijakazi Abdalla /Maelezo. 09/07/2021.
Kufuatia agizo lilitolewa na Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Hemed Suleiman Abdulla la kutaka mnada wa nazi kufanyika katika Soko la Kibandamaiti wafanyabiashara wa Soko la Jumbi wamelalamika na kuiomba Serikali kuurudisha mnada huo katika soko hilo ili kuondosha usumbufu wanaopata
Wakizungumza na Waandishi wa habari wa wafanyabiashara hao katika soko hilo wamesema wanapata usumbufu kutokana na soko la Kibandamaiti ni dogo halikidhi kutoa huduma za mnada ukilinganisha na Soko la Jumbi
“Soko la Jumbi ndio soko kubwa kwa mnada kuliko masoko yote yalokuwepo Mkoa wa Mjini kwa kuwepo nafasi kubwa ya kufanya mnada”, walifahamisha wafanyabiashara hao.
Wameeleza kuwa hawapingi agizo la Serikali kuondosha mnada katika soko hilo lakini imekuwa ni tatizo kwa wafanyabiashara kuhamishwa minada katika maeneo yenye nafasi na kupelekwa katika sehemu ambazo hazitoshelezi.
Hata hivyo wameiomba Serikali kuboresha mazingira ya soko la Jumbi kwa kuwekewa vyoo na mahitaji mengine kwa lengo la kutoa huduma nzuri.
Aidha wameitaka Serikali kuwashirikisha wafanyabiashara wakati wa kufanya maamuzi ili kuepukana migogoro na mivutano katika masoko.
“Maisha yetu yanaendeshwa na kufanya biashara hivyo kuwepo kwa mivutano kati yetu katika masoko imekuwa zinadhorotesha maisha yetu katika familia”, wamesema Wafanya biashara hao.