Afisa Mtendaji Mkuu wa taasisi ya Benjamini Mkapa Foundation, Dkt.Hellen Senkoro akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam akitoa taarifa ya kuwepo kwa mdaharo wa kumbukizi ya maisha ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamini Mkapa.
(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)
***********************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu anatarajia kuwa mgeni rasmi katika mdaharo wa kumbukizi ya maisha ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamini William Mkapa utakaofanyika siku ya tarehe 14 Julai mwaka huu Mlimani City Jijini Dar es Salaam.
Mdaharo huo umeandaliwa na taasisi ya Benjamini Mkapa Foundation kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam,Afisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Dkt.Hellen Senkoro amesema kuwa mdaharo huo ni sehemu ya kuenzi mchango wa hayati Benjamini Mkapa kwenye taifa hili, Afrika na Duniani, ambao utafanyika chini ya kauli mbiu isemayo “HAYATI BENJAMINI MKAPA:MWAKA MMOJA TANGU ATUTOKE, TUNAYAKUMBUKA MAISHA YAKE, TUNAENZI URITHI WAKE”.
Amesema viongozi mashuhuriwanaotarajia kushiriki kupitia uwepo wao binafsi au kwa njia ya mtandao ni pamoja na aliyekuwa Rais wa 42 wa Marekani Mhe.Bill Clinton, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Mhe.Tonny Blair, aliyekuwa Rais wa Nigeria Mhe.Olegesun Obasanjo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa wa kupambana na UKIMWI (UNAIDS) Bi.Winnie Byanyima ambao wote kwa pamoja watatoa salaam zao kwa njia ya video wakielezea walivyomfahamu Hayati Benjamini Mkapa katika kushirikiana nae katika kazi mbalimbali za kuleta maendeleo Duniani hususan katika Bara Afrika na nchini Tanzania.
“Viongozi wengine wa kitaifa ambao watakaohudhuria mdaharo huo ni pamoja na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe.Dkt.Hussein Mwinyi,Viongozi wakuu wa Serikali, Marais na Viongozi Wastaafu kutoka Tanzania Bara na Visiwani, Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa hapa nchini, Wakuu wa Taasisi mbalimbali za Umma pamoja na Asasi za kiraia na viongozi wa dini”. Amesema Dkt.Senkoro.
Aidha Dkt.Senkoro amesema licha ya kuwa na mdaharo pia Rais Mhe.Samia atazindua mfuko maalumu wa Taasisi “Endowment Fund”.Mfuko huo unaanzishwa chini ya Taasisi ya Benjamini Mkapa, una lengo la kuongeza chachu katika kuimarisha huduma za afya nchini.