************************************
Na. Damian Kunambi, Njombe.
Imeelezwa kuwa katika kipindi cha siku 100 za rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hasani zimekuwa na neema kwa wanakijiji cha Liughai kilichopo katika kata ya Luilo wilayani Ludewa mkoani Njombe kwa kutengewa kiasi cha shilingi milioni 381 kwa ajili ya mradi wa maji.
Hayo ameyasema mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga alipofanya ziara kijijini hapo na kuongeza kuwa aliitambua changamoto hiyo wanayoipata na kuiwasilisha serikalini na hatimaye ombi limefanyiwa kazi.
Amesema maji safi na salama ni muhimu sana kwa kila mwanadamu na ndio maana alihakikisha kuwa anafikisha kilio cha wananchi wa kijiji hicho ili liweze kupatiwa ufumbuzi.
“Rais mama Samia ni rais msikivu na anayejali wananchi, na ndiomaana suala hili limeweza kupatiwa ufumbuzi wa haraka kwakuwa serikali nayo inatambua umuhimu wa maji”, Alisema Kamonga.
Aidha kwa upande wa wanakijinji hao wamepokea kwa furaha taarifa hizo na wamempongeza mbunge huyo kwa kuwajali maana tatizo hilo linawasumbua kwa muda mrefu.
Leah Haule ni mkazi wa kijiji cha Liughai ameaema maji ni tatizo kubwa sana katika kijiji hicho kwani maji wanayoyatumia ni machafu na yanapatikana kwa umbali mrefu.
Ameongeza kuwa taarifa alizoleta mbunge ni njema sana kwao ameonyesha ni kwa jinsi gani mbunge huyo anawajali hivyo wanamuona ni mbunge anayepaswa kuongoza kwa muda mrefu maana ana nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo.
Katika hatua nyingine mbunge huyo baada ya kuwasili katika kijiji cha Lifua katani humo alivamiwa na kundi la wanafunzi mkutanoni hapo wakidai wamechoka kukaa chini hivyo wanahitaji msaada madawati.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake Elisha Kikoti amesema kuwa shule yao ina wanafunzi 297 na inamadawati 47 kitu ambacho kinapelekea kukaa chini.
Amesema hali hiyo inawapelekea kuwa wachafu muda wote kwakua inawalazimu kukaa chini.
Aidha kwa upande wa mbunge huyo amesema kuwa mazingira hayo yanasikitisha sana kwa wanafunzi na yanaweza kusababisha wanafunzi kutokuwa wasikivu darasani.
Ameongeza kuwa ili kutatua changamoto hiyo atahakikisha anazungumza na waziri wa maliasili ili aweze kutoa kibali cha kuvuna mbao katika eneo ambalo lipo katika miliki ya wananchi.
“Tatizo hili linawapa wakati mgumu sana wanafunzi kwani wanapokaa chini kunawafanya washindwe kuwa na miandiko mizuri”, alisema Kamonga.
Elias Ngatunga ni mmoja wa vijana wa kijiji hicho ambapo amefurahishwa na kitendo cha mbunge huyo kuguswa na changamoto hiyo na kuahidi wao kama vijana kuonyesha ushirikiano katika kukata mbao hizo endapo kibali kitatoka.