Mkuu wa kitengo cha mahusiano AUWSA,Masoud Katiba akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake(Happy Lazaro).
………………………………………………………………..
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha.Mamlaka ya maji Safi na usafi wa mazingira (AUWSA) jijini Arusha imeendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi sahihi ya huduma za maji .
Hata hivyo ,mamlaka hiyo imewataka wananchi wake kufika katika ofisi hizo kwa ajili ya kueleza changamoto zao na kuweza kupata elimu juu ya matumizi sahihi ya huduma hiyo.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa kitengo cha mahusiano ya umma AUWSA ,Masoud Katiba wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Amesema kuwa ,wamekuwa wakishirikiana na wateja kwa karibu sambamba na kuwatembelea katika makazi yao na kuweza kutoa huduma hiyo na kutatua changamoto pale zinapokuwepo.
Katiba amesema kuwa,wananchi wengi wamekuwa wakilalamikia kupanda kwa bili ya maji katika mita zao kitendo ambacho wanailalamikia mamlaka hiyo,ambapo amesema hiyo ni kutokana na wengi wao kutokuwa na elimu ya kutosha kwani matatizo mengi yaliyopo yanatoka kwenye mitandao yao.
“tumekuwa tukitoa elimu kwa wananchi kupitia dawati la huduma kwa wateja ambapo wamekuwa wakielezea changamoto zao za maji na sisi tunazifanyia kazi kwa haraka ikiwemo kupeleka wataalamu katika maeneo hayo ili kuweza kubaini changamoto ilipo.”amesema Katiba.
Katiba amesema kuwa, wamekuwa wakiwashauri wananchi kufika katika mamlaka hiyo,kwa ajili ya kupata huduma sambamba na kuelezea changamoto zao na hatimaye wataalamu kuweza kufika katika maeneo yao na kufanyiwa ukaguzi kulingana na malalamiko yao.
Amesema kuwa, bado kuna changamoto kubwa ya elimu kwa wananchi wake ambapo bado wanaendelea kutoa elimu zaidi kuhusiana na huduma hiyo ili kuwawezesha wananchi wake kupata huduma nzuri na inayoridhisha.