Mkurugenzi Msaidizi wa Uendelezaji Mazao, Pembejeo na Ushirika kutoka Wizara ya Kilimo Beatus Malema (Katika) Mwenyekiti wa Mwavuli wa Kilimo Hai Tanzania (TOAM), Dk.Mwatima Juma, (Kushoto) Mtaribu wa Kongamano hilo, Vida Makamba kutoka Kampuni ya AMMI
**************************
Na Selemani Msuya
WAKULIMA nchini wameshauriwa kujikita kwenye kuzalisha mazao yatokanayo na kilimo hai kwa kuwa kinachangia ajira, uchumi, chakula, afya na utunzaji wa mazingira.
Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Mwavuli wa Kilimo Hai Tanzania (TOAM), Dk.Mwatima Juma wakati akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuhusu Kongamano la Pili la Kitaifa la Kilimo Hai litakalofanyika Jijini Dodoma Oktoba mwaka huu.
Dk.Juma alisema mazao yanayotokana na kilimo hai ndio hitaji la dunia hivyo ni wakati wa wakulima kuongeza kasi kwenye uzalishaji wa mazao hayo ili kuendana na hitaji hilo.
“Oktoba mwaka huu tutakuwa na kongamano la pili la kilimo hai, pamoja na mambo mengine yatakayojadiliwa ni vema tukatoka na kauli moja kuhusu uhamasishaji kilimo hai kwa kuwa hali ilivyo sasa tunaendelea kumalizana kwa kutumia mazao ambayo sio salama kwa afya zetu,” alisema.
Alisema iwapo wakulima watajikita kwenye kilimo hai wataweza kuchochea ukuaji wa uchumi, kulinda afya, kuongeza uzalishaji, ajira na kutunza mazingira hali ambayo kwa njia za kilimo cha kutumia pembejeo za madukani halipatikani.
Dk. Mwatima alisema hadi sasa mwikio wa wakulima kujikita katika kilimo hai ni mdogo hivyo ni vema Serikali ikaongeza nguvu zaidi eneo hilo kwa kuwa ni fursa ya kukuza uchumi na ajira.
“Kilimo Hai kina tafsiri nyingi sana lakini uhalisia wake ni kwamba kilimo hai sio kwa mimea hata kwa mifugo na mwenendo wa maisha yetu. Hivyo kongamano hili litajikita kujadili umuhimu wa kilimo hai kwa Taifa,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema Kilimo Hai kitalifanya Taifa kuwa huru na sio tegemezi kwenye mbegu, miche na bidhaa zote ambazo zinahusika kwenye mchakato wa kilimo.
Mwatima alisema Kilimo Hai kinatumia bidhaa kutoka shambani katika kurutubisha mazao huku kikiruhusu kilimo mchanganyiko hivyo juhudu zinahitajika kwenye kutoa elimu ili wakulima waweze kunufaika nacho.
Alisema mabadiliko ya tabianchi ambayo yanalalamikiwa katila ulimwengu wa sasa yanachangiwa na jamii kuachana na kilimo hai na kuegemea kilimo cha kutumia pembejeo kutoka nje.
“Kilimo Hai kinarejesha uhalisia wa binadamu na kilimo ambapo kitaweza kuchangio kukabiliana na maradhi kama saratani na mengine mengi,” alisema.
Dk. Mwitima alisema kongamano hilo la Kilimo Hai litashirikisha wadau kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (FAO), Taasisi ya Kilimo Endelevu (SAT), Shirika la Swisis Aid, Chuo cha Kilimo Sokoine (SUA), Asasi ya Kilimo ya Island Peace, Shirika la GIZ, Mtandao wa Bionuai wa Tanzania (TABIO) na St. Joseph.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Uendelezaji Mazao, Pembejeo na Ushirika kutoka Wizara ya Kilimo Beatus Malema alisema Serikali ipo pamoja na wadau wote ambao wanapigania na kuhamasisha kilimo hai kwa kuwa kina faida kwa taifa.
Malema alisema katika kuunga mkono mchakato huo wizara ya Kilimo imeanzisha dawati la Kilimo Hai ambalo linaratibu shughuli zote za kilimo hicho.
“Kilimo hai kinachochea utumiaji wa mbegu asili jambo ambalo Serikali inasisitiza ili kuongeza uzalishaji kwenye sekta hiyo muhimu kwa uchumi wan chi,” alisema.
Naye Mtaribu wa Kongamano hilo, Vida Makamba kutoka Kampuni ya AMMI alisema kongamano hilo linatarajiwa kushirikisha wadau wa Kilimo Hai 300 kutoka ndani na nje ya nchi.