……………………………………………………………….
Nimekuwa nikifuatilia kwa karibu harakati zenu za kisiasa za kujinadi kwa wadau kwa njia ya makongamano na mitandao ya kijamii.
Hivyo kama mlezi na msimamizi wa sheria ya vyama vya siasa napenda kutumia fursa hii kuwakumbusha kuwa, nikiwa mlezi wa vyama vya siasa na msimamizi mkuu wa utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa inayoratibu usajili na shughuli za vyama vya siasa, nina wajibu wa kuwaasa kama vyama vya siasa kuhusu mwenendo wa shughuli zenu za kisiasa.
Natambua kuwa mojawapo ya malengo na majukumu ya chama cha siasa ni kunadi sera zenu ili zikubalike na wananchi. Vivyo Hivyo, katika kutekeleza suala hili vyama vya siasa vitakuwa vinaongea na wananchi kwa njia mbalimbali ili mradi hazikinzani na Sheria za nchi. Kwa muktadha huo, natumia fursa hii kuviasa vyama vya siasa kuzingatia sheria za nchi katika shughuli zenu za kila siku, ili kuhakikisha mnafanya kazi katika mazingira ya amani na utulivu. Aidha, vyama vya siasa vipo katika jamii ya Watanzania ambayo ina watu ambao ni wanachama wa vyama mbalimbali na wengine hawana vyama, hivyo ni vyema vyama vya siasa vikafanya shughuli zake kwa kuzingatia maslahi na haki za watu wengine kwa ujumla wake.
Ili kudumisha amani, utulivu na kuzingatia maslahi na haki za watu wengine katika jamii, nina visihi vyama vya siasa kufanya siasa za kistaarabu na kuvumiliana kukuza dhana ya kisiasa. Siasa za kistaarabu maana yake ni pamoja na kufanya siasa kwa kuheshimu sheria za nchi, kuepuka lugha za uchochezi, dhihaka, dharau, vitisho na matusi. Namalizia kwa kusisitiza kuwa, demokrasia inatekelezeka vyema mahali ambapo wadau wanaheshimu sheria za nchi, wanafanya siasa za kistaarabu.