*****************************
NJOMBE
Serikali Njombe imelitangaza rasmi kaburi la Mzee Antony Mwandulami maarufu Dr Mwandulami kuwa kivutio cha 12 cha utalii kilichopo katika wilaya hiyo na kuwataka watalii kutoka ndani na nje ya nchi kutembelea na kumuenzi nguli huyo wa masuala ya tiba asilia nchini.
Miaka ya 2000 Kutoka kijiji cha Itunduma kilichopo kata ya Mtwango mkoani Njombe mzee Mwandulami ambaye ni mtaalamu wa tiba mbadala na asilia ,mwenye hospitali ya kisasa nyumbani kwake anakoendeshea tiba asilia ,alijipatia umaarufu mkubwa kwa kuanza kujenga kaburi la mamilioni ya fedha akitaka baada ya kifo chake na wake zake wapumzishwe hapo na kufanya kuwa kivutio.
Akiwa katika hatua za mwisho za kukamilisha ndoto aliyoishi nayo kwa muda mrefu ya kuandaa makazi yake ya milele ugonjwa ukamshambulia na Umauti kumkuta akiwa katikati ya vita ya kuokoa maisha yake jambo ambalo limeacha simanzi kubwa kwa wengi.
Kutokana na mchango wake katika masuala ya maendeleo ,wakati wa mazishi Serikali ikatangaza kukitambua na kuliorodhesha kaburi hilo kuwa moja kati ya vivutio 12 vya kitalii vilivyopo halmashauri ya wilaya ya Njombe huku Katibu mkuu wa shirika la dawa asilia nchini (TRAMEPRO)Boniventura Mwalongo akisema walikuwa katika hatua za mwisho za kisheria za kumtambua mzee Mwandulami kuwa nguli na Kuhani wa tiba asilia Africa.
Awali akiondoa sintofahamu ya sababu ya kifo,Tarik Hamza ambaye ni mjukuu akisoma historia ya Marehemu amesema mzee Mwandulami amefariki kwa tatizo la uvimbe tumboni na kuwaomba ndugu jamaa na marafiki kuwa nao katika kipindi hiki kigumu ya kuondokewa na mpendwa wao
Baadhi ya waombolezaji akiwemo Salum Mulumbe,Edward Mgaya na Ernest Musa ambaye ndiye fundi wa ujenzi wa kaburi hilo aliyeanza kulijenga mwka 2000 wamemuelezea marehemu kama mtu wa tofauti sana aliyekuwa mwepesi kusaidia jamii zinazoteseka .