………………………………………………………………….
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro amezindua Utalii wa Faru katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi iliyopo Wilayani Same, Kilimanjaro. Uzinduzi huo umeshuhudiwa na Naibu Waziri wa Maliasili, Mary Masanja, RC wa Tanga, Adam Malima na DC wa Same, Edward Mpogolo.
Waziri Dk Ndumbaro amesema Hifadhi ya Mkomazi ni muhimu ingawa ina changamoto ya upatikanaji wa maji kwa ajili ya wanyama na binadamu ambapo ameziagia Mamlaka zinazohusika kuhakikisha mabwawa yanachimbwa mara moja ili wanyama wasiende umbali mrefu kutafuta maji.
Dk Ndumbaro pia ameielekeza mamlaka ya wanyamapori kuhamisha baadhi ya Nyumbu waliopo kwenye Hifadhi ya Serengeti kuletwa Mkomazi ili kukidhi haja ya wageni kwani kwa sasa Mkomazi haina aina hiyo ya wanyama.
” Tunataka kuongeza idadi ya watalii kufika Milioni 5 ifikapo mwaka 2025 na kupata mapato yatokanayo na utalii kiasi cha Sh Bilioni 6 kutoka kiasi cha Sh Bilioni 2.6 kwa sasa,”Amesema Dk Ndumbaro.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Same, Edward Mpogolo ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu Utalii huo huku akisema anaamini utachochea ukuaji wa uchumi wa Same.
“Nimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu Faru hawa kutumika kwa Utalii kwenye Hifadhi ya Mkomazi, kwa kuruhusu Utalii wa Faru kutaongeza Watalii na Mapato kwa Serikali, Niwaombe Wananchi wa Same kuchangamkia fursa hiyo kwa kujenga Hoteli nzuri,” Amesema DC Mpogolo.