Home Mchanganyiko WIZARA YA HABARI YAMPONGEZA RAIS SAMIA, YAJA NA NGUZO TANO

WIZARA YA HABARI YAMPONGEZA RAIS SAMIA, YAJA NA NGUZO TANO

0

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa akitoa maelekezo leo Julai 06, 2021 wakati wa kikao cha kimkakati cha Menejimenti ya Wizara hiyo kujadili mikakati ya utekelezaji wa kazi za Wizara.

Katibu wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi akitoa maelezo ya awali kwa Mhe. Waziri, Innocent Bashungwa na Naibu wake Mhe. Pauline Gekul leo Julai 06, 2021 wakati wa kikao cha kimkakati cha Menejimenti ya Wizara hiyo kujadili mikakati ya utekelezaji wa kazi za Wizara.

Viongozi Wakuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakiongoza kikao cha kimkakati cha Menejimenti ya Wizara hiyo kujadili mikakati ya utekelezaji wa kazi za Wizara.

Baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Habari leo Julai 06, 2021 wakijadili mikakati ya utekelezaji wa kazi za Wizara.

******************************

Na John Mapepele, WHUSM

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa leo Julai 06, 2021 amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kumaliza siku 100 kazini kwa kishindo na mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na sekta za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mhe. Bashungwa ameyasema haya wakati akifungua kikao cha kimkakati cha Menejimenti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kilichoketi kujadili mikakati ya utekelezaji wa kazi za Wizara kwenye kipindi cha miezi sita ili kuleta mapinduzi makubwa kwenye sekta na wadau mbalimbali.

“Ndugu zangu dhamira ya kikao hiki ni kujipanga kimkakati ili kumsaidia Mhe. Rais kwenye dira aliyotuelekeza katika kipindi hiki ili matokeo yaliyokusudiwa yaweze kupatikana.” Ameongeza Mhe. Bashungwa

Amesisitiza kuwa Wizara yake itaendelea kujenga utamaduni wa kukutana na kujadili mikakati ya kuendeleza sekta zote ambapo amesema vikao hivi vitakuwa ni sehemu ya kufanya tathimini na ufuatiliaji wa utekelezaji wa maelekezo ya Viongozi Wakuu wa nchi na kazi mbalimbali za Wizara.

Awali, Katibu Mkuu wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi akitoa maelezo ya utangulizi kwa Mhe. Waziri na Naibu wake Mhe. Pauline Gekul amezitaja nguzo tano  zitakazoongoza utekelezaji wa mikakati hiyo kuwa ni pamoja na  kuwafikia wadau mbalimbali ili kutatua changamoto, kufanya mageuzi ya kitaasisi na ya kiutendaji pamoja na kubadili mitazamo ya watendaji wa Wizara na taasisi zake, kusimamia utawala bora kwenye sekta chini ya Wizara, ujenzi wa miundombinu kwenye sekta za michezo na sanaa na uhamasishaji wa rasilimali.

Mhe. Bashungwa amesema amependa ubunifu wa kuwa na nguzo maalum zinazoongoza utekelezaji wa kimkakati uliofanywa na Mwenyekiti wa Menejimenti ya Wizara ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi, na Naibu wake Dkt. Ally Possi ambapo ametaka kila nguzo iwe na mkakati kabambe wa utekelezaji wake ili malengo yaweze kufikiwa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul amepongeza kazi zinazofanywa na Menejimenti ya Wizara na kutaka pia kuharakisha kutekeleza mikakati ya michezo kwa upande wa wananwake hapa nchini na vazi la taifa.

Baada ya kufunguliwa kwa kikao hicho mambo mbalimbali ya kimkakati yamejadiliwa na kutoka na maazimio maalum.