Afisa kilimo wa Kata ya KingerikitinHamida issa akionyesha mashine ya kisasa ya kuchakata kahawa ya kingerikiti Amcoss ambayo inaandaa kahawa bora na kutoa sukari na kuongeza thamani ya kahawa ya Wilaya ya Nyasa.picha na ofisi ya Ded Nyasa.
Picha nyingine akichambua kahawa na kuwaelekeza wakulima jinsi ya kuanikana kuchambua kahawa
……………………………………………………….
Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, imetoa mafunzo kwa Viongozi wa Vyama Tisa vya msingi vya Ushirika, namna ya kuchakata kahawa bora na kuiingiza katika soko la biashara ya kahawa ili iwe na thamani na kuuza kwa bei ya juu ili iweze kumnufaisha Mkulima.
Mafunzo hayo yametolewa hivi karibuni katika Ukumbi wa Mikutano wa Shule ya Msingi Kingerikiti, kwa Viongozi wa Vyama tisa Vya Msingi vya Ushirika na Mazao (AMCOS), na Afisa Ushirika wa Wilaya ya Nyasa Bw. Menance Ndomba, Mafunzo yenye lengo la kuhakikisha Wilaya ya Nyasa inauza kahawa bora kwenye soko , na yenye thamani kubwa kwa mlaji ili kuweza kuongeza kipato kwa wakulima wa zao la kahawa Wilayani hapa.
Bw. Ndomba amefafanua kuwa kwa Wilaya ya Nyasa, Tarafa ya Mpepo wilayani Nyasa ndio inayozalisha kwa wingi zao la kahawa, hivyo wamelazimika kutoa mafunzo ya kuchuma na kuchakata zao la kahawa kwa viongozi wa Vyama vya msingi wa mazao (AMCOS), ili kuwajengea uwezo viongozi hao ili wakawaelimishe wakulima wao jinsi ya kuandaa kahawa bora na kuifikisha katika soko, ili waweze kuuza kahawa yenye ubora na kupata fedha ili kujiletea maendeleo ya kaya, Halmashauri na Taifa kwa Ujumla.
Ameongeza kuwa, awali alitoa mafunzo kwa wakulima jinsi ya kulima kahawa bora kwa kutotumia kemikali na badala yake watumie samadi na kupanda mbegu ya kisasa, aina ya Compact ambayo hustawi katika Wilaya ya Nyasa na kumpa mavuno makubwa mkulima baada ya muda mfupi na waachane na mbegu za zamani ili waweze kujiletea maendeleo.
Amewataka wanunuzi wa Zao la kahawa kuja kununua kahawa ya Wilaya ya Nyasa, kwa kuwa ni bora, na imeandaliwa na kuchakatwa kitaalam kwa kufuata miongozo ya wanywaji, kwa kutotumia kemikali, na kuchakatwa kiwandani. Kiwanda ambacho ni kizuri na cha kisasa ambacho hata sukari ya kahawa huondolewa kwa mashine na kupata kahawa bora ambayo haina madhara kwa mtumiaji.
Naye Afisa kilimo wa Kata ya Kingerikiti Wilayani Nyasa Hamida Issa amesema wakulima wa zao la kahawa Wilaya ya Nyasa wamehamasika kulima zao la kahawa kitaalam, kwa kujifuza kupitia shamba darasa ambalo amelianzisha katika Kata hiyo kwa kuwa linawaletea mazao bora, ambayo thamani yake ni kubwa kipindi wamnapoenda kuuza mnadani na kuwaletea kipato kinachowasaidia kufanyia shughuli mbalimbali.
Aidha amesema wakulima wengi kwa sasa kahawa yao wanalima kwa kufuata miongozo ya wataalamu wa zao la Kahawa kupitia shamba darasa lililopo katika kata hiyo kwa kupanda mbegu bora aina ya Compact ambayo huzaa baada ya miaka miwili na kuifikisha kiwanda cha kuchakata kahawa kilichopo kingerikiti na kuachana na tabia ya kuchakata kienyeji kahawa hiyo na kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi.
Ametoa Wito kwa Wananchi wa Wilaya ya Nyasa kutumia mashine hiyo ya kuchakata kahawa kitaalamu na kuondoa sukari ya kahawa kwa kutumia mashine hiyo ili kujiongezea kipato kwa kuwa kahawa jinsi unavyoiandaa vizuri tangu kulima, kuchuma, kuchakata, kuanika, kuhifadhi na kuiuza ndivyo wakulima wa zao hilo watakavyonufaika na zao hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Nyasa Bw Jimson Mhagama amewataka wadau wa zao la kahawa kuja kuwekeza Wilayani nyasa kwa kulima, na kununua zao la kahawa kwa kuwa Wilaya ya Nyasa ina maeneo makubwa ya kulima na uwekezaji wa zao la kahawa ukilinganisha na Wilaya ya Mbinga, pia kahawa inayozalishwa katika Wilaya ya Nyasa ni tofauti na kahawa inayolimwa sehemu nyingine kwa kuwa wakulima wa Nyasa hulima kahawa kwa kufuata miongozo ya kitaalam na kuvuna kahawa bora kwa usimamizi wa wataalam wa kilimo Wilayani Nyasa.
Imeandaliwa na Netho C. Sichali
Afisa Habari Wilaya ya Nyasa, 0767417597