*********************
Na Silvia Mchuruza,
Bukoba,
Serikali Mkoani Kagera imeahidi kuchukua hatua za kisheria kwa Halmashauri zinazobadili matumizi ya ujenzi wa miradi ya maendeleo na kusababisha miradi kukwama.
Kauli hiyo imekuja kufuatia agizo la mkuu wa mkoa wa Kagera meja Jenerali Charles Mbuge kuagiza Halmashauri ya Bukoba kuacha tabia ya kubadili matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo zinazotolewa na serikali na kuzielekeza katika matumizi ya kawaida.
Akizunguza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Kagera katika kikao maalum cha kujadili taarifa ya mkaguzi na mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali(CAG) katibu tawala msaidizi Mkoani Kagera Projectus Rubanzibwa amesema kuwa changamoto ya kubadili matumizi ya fedha za miradi katika halmashauri hiyo imetajwa katika taarifa ya mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali CAG kwa mwaka wa fedha 2019/ 2020.
Rubanzibwa ameeleza kuwa serikali itaanza kuchukua hatua za kisheria kwa halmashauri zinazofanya vitendo vya kubadili matumizi ya ujenzi wa miradi ya maendeleo na kusababisha miradi hiyo kukwama na kuzorota kwa maendeleo ya halmashauri hizo.
Aidha kwa upande wake kaimu mwenyekiti wa Halmashauri ya Bukoba Privatus Mweleka amesema kuwa halmashauri hiyo inajivunia kupata hati safi kwa takribani miaka minne mfulilizo na kuomba watendaji wa halmashauri hiyo kuendeleza ushirikiano ili kuwa hati safi zaidi.
Naye diwani wa kata ya Nyakibimbili Vicent John amesema kuwa suala hilo la kujadili matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo iliyolengwa si sahihi kwani urudisha maendeleo ya wananchi nyuma na kuleta lawama kwa serikali.
Hata hivyo diwani wa kata ya Karabagaine Samweli Richard Makwabe na Michael Peter Lubisi diwani wa kata Ibwera wamesema suala hilo linachelewesha maendeleo na kuwa fedha za miradi zikipangwa kufanya maendeleo lazima zifanye maendeleo lengwa na si vingine