Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akiongea na Wanaushirika wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani Julai 03,2021 katika Viwanja vya Nanenane, Mkoani Tabora
Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akiuliza jambo katika mabanda ya maonesho ya Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani, (kulia) ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) Bi. Theresia Chitumbi katika Viwanja vya Nanenane, Mkoani Tabora
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani mkoani Tabora.
……………………………………………………………..
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amesema Serikali ina dhamira ya dhati kuhakikisha kuwa Vyama vya Ushirika vinaimarika na wakulima wanapata tija na manufaa ya shughuli za uchumi zinazoendeshwa kwenye Vyama vya ushirika.
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani Julai 03, 2021 yaliyozinduliwa Julai 29, 2021 viwanja vya Nanenane Ipuli Mkoani Tabora.
Mhe. Kassim Majaliwa ameeleza kuwa Ushirika ni Sekta muhimu yenye mchango mkubwa kwa Taifa ambayo inahusisha shughuli za uchumi ikiwemo Kilimo, uvuvi, ufugaji na Nyanja nyingine za uchumi ambazo zote hutoa ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa. Hivyo, amewataka Viongozi na watendaji wa Sekta ya Ushirika kuhakikisha kuwa Vyama vya Ushirika vinaendeshwa kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu na kusimamia Vyama kwa misingi ya uadilifu ili kuondokana na changamoto ambazo zimekuwepo zinazoharibu taswira ya Ushirika.
“Lazima tuzilinde mali za Ushirika jukumu tulilonalo viongozi wa Ushirika ni kusimamia mali za Ushirika na kuheshimu dhamana tulizopewa na wanaushirika,” alisema Waziri Mkuu
Akizungumzia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala Waziri Mkuu amesema mfumo huo ni mkombozi kwa wakulima kwani mkulima anapata fursa ya kupata bei yenye ushindani kupitia minada ya ununuzi ambayo mara nyingi ni ngumu kuipata kwa walanguzi. Hivyo, ameitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuendeleza juhudi za kuelimisha kuhusu mfumo huu na kuhakikisha hata maeneo yenye changamoto na mfumo elimu itolewe ili wakulima waelewe manufaa ya mfumo.
Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege amesema Tume inaendelea kuunga mkono Juhudi za kufufua viwanda ili kuongeza thamani za mazao yanayozalishwa na wakulima. Ameongeza kuwa kwa kipindi cha mwaka jana tayari viwanda vitatu vinavyomilikiwa na Vyama vya Ushirika vimeanza kufanya kazi akivitaja viwanda vinavyomilikiwa na KACU, Chato na Mbogwe jambo ambalo linasaidia kuongeza bei ya mazao na ushindani wa soko.
Aidha, Dkt. Ndiege ametoa wito kwa vyama vya Ushirika kuitumia Benki ya Ushirika ya KCBL ambayo tayari imeanza kazi kuanzia Novemba mwaka jana. Mrajis ameongeza kuwa Benki hiyo ni mahususi kwaajili ya wanaushirika na tayari imeanza kupata faida.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika (TFC) Bi. Theresia Chitumbi ameeleza Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Ushirika duniani 2021 isemayo “Ushirika tujijenge upya kwa ubora na tija” inalenga kuonesha ustahimilivu wa Vyama vya Ushirika katika kusaidia na kutoa michango ya utu kwa jamii katika kipindi cha majanga mbalimbali kama mabadiliko ya tabia nchi, uharibifu wa mazingira na hali ya hewa. Kauli mbiu hiyo inalenga kuchochea vyama vya ushirika kutumia nguvu yake ya umoja, maadili yake na tunu katika kutafuta suluhu ya changamoto.
Mwenyekiti huyo ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuamini ushirika kama taasisi zenye uwezo wa kuchochea maendeleo ya uchumi pamoja na jitihada kubwa za urejeshaji wa mali za Ushirika zilizokuwa zimeuzwa na kuporwa kiholela zimechukuliwa bila utaratibu zikiwemo nyumba za makazi, maghala, viwanda na viwanja. Akiongeza kuwa wanaushirika wanaimani kuwa Serikali itaendelea na zoezi hilo la kutafuta na kuzirudisha mali za ushirika ni endelevu.
Akielezea baadhi ya Changamoto inayovikabili Vyama vya Ushirika wa akiba na Mikopo (SACCOS) mwenyekiti amesema Vyama hivi hupokea hisa, akiba, na amana za wanachama kupitia makato ya mishahara ya watumishi husika. Hata hivyo, fedha hizo hukatwa tozo la gharama la gharama (processing fees) kwa asilimia mbili na vyama hupokea fedha pungufu za wanachama kwa kiasi cha asilimia hizo lakini hulazimika kunjazia mwanachama fedha kamili kwenye taarifa zake hivyo kusababisha vyama kuingia hasara. Pamoja na ucheleweshaji wa marejesho kutoka kwa waajiri.