…………………………………………………………
NJOMBE
Mkazi wa kijiji cha Wangama kilichopo tarafa ya Makambako wilayani Njombe Antony Mwandulami aliyejipatia umaarufu mkubwa baada ya kujijengea kaburi lake linalotajwa kugharimu mamilioni ya fedha amefariki dunia katika hospitali ya taifa Muhimbili.
TAARIFA YA JOCTAN MYEFU KUTOKA NJOMBE
Mkazi huyo aliyekuwa nguli wa tiba asilia akipewa jina la Dr Mwandulami hadi umauti unamfika anadaiwa kutibu maelfu ya watu kutoka ndani na nje ya nchi kwa kutumia miti shamba huku akimtumia mbuzi katika kupima tatizo la mgonjwa na kisha kumlaza katika hospitali ya kisasa ambayo amejenga nyumbani kwake katika kijiji cha Wangama.
Kwa mujibu wa ndugu, Dr Mwandulami alizaliwa mwaka 1951 na amefariki akiwa na umri wa miaka 69 akiwa bado katika ukarabati wa makazi yake ya milele ambapo katika kaburi hilo lenye muundo wa ghorofa likiwa na msalaba juu mithiri ya kanisa ,ndani yake kuna chumba kikubwa kimoja ambacho kina makaburi mane likiwemo lake na wake zake watatu.
Enzi za uhai wake Dr Mwandulami alisema amefanya hivyo ili kuilifanya eneo hilo kuwa la kitalii na kwamba akifa apumzishwe hapo na wake zake.
Baadhi ya ndugu wa mzee Mwandulami akiwemo Neema Mwinami na Naboti Mhapa wameeleza namna walivyoshitishwa na kifo cha ndugu yao huku pia wakieleza safari ya ujenzi wa kaburi hilo uliochukua miongo kadhaa licha ya kuwa hadi sasa haujakamilika ipasavyo.
Katika kipindi chote mzee mwandulami aliyejiandalia kaburi amekuwa mshauri na mlezi wa chama cha watalaamu wa mbadala na asilia mkoani Njombe,jambo ambalo linaonekana kuwaumiza zaidi watalaamu wa tiba asilia .Kama ambavyo Dr Kifagio ambaye ni mwenyekiti wa tiba asili na mbadala mkoa anavyoeleza.
Katika Nyumba ya Dr Mwandulami kuna mambo makubwa mawili ambayo yalikuwa ya kustaajabisha ambayo ni mbuzi wawili ambao walikuwa na jukumu la kupokea wageni na kutafsiri tatizo la mgonjwa pamoja na uwepo wa kaburi refu lenye msalaba mithiri ya jengo lla kanisa .