…………………………………………………………………
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
MBUNGE wa viti maalum mkoani Pwani ,Subira Mgalu pamoja na UWT Kibaha Mjini, amekemea baadhi ya wanasiasa pinzani wanaotoa sauti kinzani kumshinikiza Rais Samia Suluhu ,kuhusu mabadiliko ya katiba kuwa ,wasijaribu kumtingisha ,kwani kibiriti kimejaa na njiti zake zinawaka .
Ameeleza wanawake wa UWT na watanzania wanaolitakia Taifa mema wapo nyuma yake na hawatakubali kuona anabezwa ,anashinikizwa wala kupewa amri .
Akizungumza katika kongamano lililoandaliwa na UWT Kibaha Mjini ,kupongeza siku 100 na hotuba aliyoitoa Rais Samia kwa wanawake pale Dodoma ,Juni 8 mwaka huu, Mgalu alieleza ,Rais apewe nafasi kuendeleza Yale aliyoyaacha Rais wa awamu ya tano marehemu John Magufuli .
Alitoa rai watu hao wapuuzwe kwa maslahi ya nchi na kuendelea kulinda amani iliyopo.
“Ndio kwanza Rais amefikisha siku 100 ,badala ya kupongeza aliyoyafanya hadi sasa ,wapo baadhi ya wanasiasa pinzani wanajitokeza kuanza kushinikiza masuala ya katiba, ameshasema katiba ina umuhimu wake ,apewe nafasi kutatua changamoto za watanzania katika sekta mbalimbali “
Hata hivyo ,alimpongeza Rais Samia, kwa bajeti ya kwanza kupitishwa bungeni kwa asilimia kubwa,huku akishukuru majimbo kupokea milioni 500 kila jimbo ambapo Pwani imeshapokea bilioni 4.5 kwa majimbo Tisa.
Pia imetolewa bilioni 100 ili kukamilisha maboma ya vituo vya afya 1,500 nchini na zahanati hatua ambayo inahitaji pongezi.
Alikadhalika Mgalu alimpongeza Rais kwa hatua ya kutoa maelekezo ya kuunganishwa umeme kwa 27,000 mjini na vijijini ,Bima ya afya kwa kaya zeenye kipato kidogo bilioni 149 ,mikopo kwa vijana vyuoni bilioni 570 na kutatua kero ya madai ya wafanyakazi wastaafu mifuko ya hifadhi ya jamii serikali inalipa tilioni 8 kwa utaratibu wa kutoa hati fungani isiyokuwa na cash.
Nae mwenyekiti wa UWT Kibaha mjini ,Elina Mgonja aliwaomba wanawake wamuunge mkono Rais Samia kwa kazi kubwa ambayo ameanza kuionyesha ndani ya siku 100 kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ametaka wanasiasa hao wasimsumbue mama na kusababisha kumuondoa katika reli .
Akielezea kongamano hilo, Mgonja alisema wamezindua ujenzi wa jengo duka maalum la kuuzia biashara na darasa la ujasiriamali ili kumkwamua mwanamke kiuchumi .
Alisema ,maelekezo yaliyotolewa Dodoma kupitia mkutano wa wanawake wao wanafanya kwa vitendo na kumhakikishia mwenyekiti wa CCM Taifa kuwa wataendelea kumshika mkono mwanamke wa Kibaha ili kujiinua kimaendeleo.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kibaha, Sara Msafiri ambae alimwakilisha mkuu wa mkoa wa Pwani ,Aboubakar Kunenge ,Sara alisema vikundi vya ujasiriamali hufa kutokana na kukosa mshikamano ,amewapongeza wilaya hiyo kuwa na Umoja na mshikamano.
Alisema hitaji la watanzania ni kutatuliwa changamoto zao ,kutatua migogoro mbalimbali ya kijamii ,kiuchumi na sio katiba kwasasa ukizingatia nchi imetoka kupata msiba mkubwa wa kuondokewa na Rais madarakani ,Hii ni bado muda mfupi sana kushinikiza mambo ambayo yanahitaji muda .
Makamu mwenyekiti wa halmashauri ya Mji wa Kibaha ,Selina Wilson alisema, kwa kutambua vikundi vya ujasiriamali, halmashauri imetoa milioni 600 ndani ya miezi sita ikiwa ni asilimia 60 kwa mikopo ya akina mama.
Katika uzinduzi wa ujenzi wa duka la kibiashara Mgalu amechangia matofali 500,mbunge Silvestry Koka mifuko 50 ya saruji,madiwani viti maalum mifuko 250 ya saruji na sh.500,000 kutoka kwa mwenyekiti wa halmashauri