Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongela akimkaribisha Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) kuzungumza na Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa mikoa ya Tanzania Bara
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akizungumza na Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa ya Tanzania Bara (hawapo pichani)
***************************
Na Evaristy Masuha-Dodoma
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amewaomba Wakuu wa mikoa na Makatibu Tawala wa mikoa kushirikiana katika usimamizi wa miradi ya maji nchini.
Mhe. Aweso amesema hayo katika kikao cha mafunzo ya uongozi kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa ya Tanzania Bara kinachofanyika jijini Dodoma.
Amesema Wizara ya Maji imedhamiria kuhakikisha lengo la kumtua mama ndoo ya maji linafikiwa kama lilivyoelekezwa na serikali.
“Niwaombe viongozi tushirikiane kwa dhati kuhakikisha tunaondoa changamoto zote za upatikanaji wa huduma ya majisafi. Peke yetu hatutaweza.” Aweso amesema.
Pamoja na hilo amepokea mapendekezo mbalimbali kutoka kwa viongozi hao wa mikoa na kuwaahidi kuyafanyia kazi.
“Kuhusu kuwa na utaratibu wa wadau wa maji kukutana na kujadili masuala mbalimbali yanayohusiana na sekta ya maji ni jema sana.
Naomba nipokee ushauri wenu wa jinsi ya kulitekeleza ili liwe endelevu. Isiwe ni maelekezo ambayo yanaweza kubadilishwa na kiongozi mwingine. Liwe ni muongozo rasmi na utamaduni ili hata kiongozi ajaye, afanye hivyohivyo” Aweso amesema.
Amesisitiza kuwa Wizara ya Maji haitakuwa kikwazo katika kufikia malengo. Amezitaja baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Wizara ili kuimarisha usimamizi wa miradi ya maji kuwa ni pamoja na uamuzi wa kuingia makubaliano na Chuo cha Maji ili kuwatumia wahitimu wa chuo hicho katika usimamizi na uendeshaji wa miradi ya maji nchini.
Wakuu hao wa mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa ya Tanzania Bara wanashiriki mafunzo ya uongozi Jijini Dodoma.