Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof Kitila Mkumbo akizungumza na Wafanyakazi wa wizara wakati wa kikao kazi kilichofanyika Julai 2,2021 jijini Dodoma kilichokuwa na lengo la kuweka mikakati na mipango ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Naibu Katibu Mkuu, Dk Harshil Twaibu Abdallah akiongea na wafanyakazi na Watendaji wa Wizara ya Viwanda na Biashara wakati wa kumkaribisha Mhe Waziri Prof Kitila Mkumbo aweze kuongea na watumishi wa Wizara hiyo Julai,2 2021 jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu ndugu Issa Ng’imba akitoa utambulisho wa watumishi kwa Mhe. Waziri Prof Kitila Mkumbo katika kikao kazi kilichofanyika Julai,2,2021 jijini Dodoma
Sehemu ya wafanyakazi na watendaji wa Wizara ya Viwanda na Biashara wakimsikiliza Waziri wa wizara hiyo,Mhe Prof Kitila Mkumbo kwenye kikao kazi kilichofanyika jijini Dodoma.
…………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
\WAZIRI wa Viwanda na Biashara Prof.Kitila Mkumbo, amesema wanapanga kuzihuwisha sera zote zilizopitwa na wakati ili ziendane na wakati uliopo.
Prof. Mkumbo ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa wizara hiyo kwa mara ya kwanza toka ateuliwe katika nafasi hiyo na Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema kuwa wizara yake inapanga kuhuwisha sera zote zilizopitwa na wakati ili kuweka mazingira rafiki ya ufanyaji biashara.
“Nimewaelekeza wenzangu lazima tuhuwishe sera zote katika wizara ya Viwanda na Biasahara zilizopitwa na wakati na iwe mwisho kuishi na sera zilizopitwa na wakati”amesema Prof. Mkumbo
Prof.Mkumbo amesema kuwa jukumu la kwanza la kila wizara ni sera na siyo kuendelea kukaa na zile ambazo zimepitwa na wakati.
“Tusifanye majukumu ya wenzetu tufanye kazi zinazaotuhusu sisi kama wizara nataka yale yaliyondani ya uwezo wangu tuyafanyie kazi”amesema
Hata hivyo amesema kuwa ni lazima wizara izifanyie marekebisho sera pamoja na sheria ili kubaini zenye changamoto na kuzifanyia kazi.
Pia amesisitiza kuwa ni lazima watumishi wa wizara hiyo kuwa wa kwanza kubaini mapungufu yaliyopo katika sera na sheria na siyo kuwaachia wafanyabiashara.
“Lazima hili mlifanye nyie katika idara yenu ya sheria kutambua changamoto zilizopo katika sera na sheria zetu ili kuzifanyia marekebisho kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika sekta ya viwanada na biashara”amesema
Aidha Prof.Mkumbo amewataka watumishi wa wizara hiyo kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sera, sheria na taratibu na wanapoona kuwa kuna upungufu hawanabudi kumshauri waziri.
Prof. Mkumbo amesema kuwa hivi sasa moja katika kero inayovikabili viwanda nchini ni uhaba wa malighafi kwa ajili ya uzalishaji bidhaa mbalimbali.
“Viwanda vyetu vinafanya kazi chini ya kiwango kwasababu hatuna malighafi za kutosha, viwanda vyetu vingine vimefungwa na vingine vinazalisha kwa muda mfupi tuu”amesisitiza Prof. Mkumbo