Meneja Rasilimali Watu (HR) wa Shirika la Empower Society Transform Lives (ESTL) linalojishughulisha na utoaji wa huduma ya uelimishaji jamii kuondokana na Ukatili wa kijinsia,ikiwemo ukeketaji, na mila potofu katika Mkoa wa Singida kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uholanzi, Philbert Swai,akizungumza na Walimu pamoja na Viongozi wa dini wa Kata ya Mukuro wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyofanyika jana Halmashauri ya Wilaya ya Singida.
Afisa Miradi wa Shirika hilo Annamaria Mashaka, akizungumza na wakunga wa jadi, wazee wa mila, mangariba, waganga wa jadi na wazee maarufu (hawapo pichani) wa Kata ya Makuro wakati wa mafunzo hayo.
Vijana wakishiriki mafunzo hayo.
Afisa Mwezeshaji wa Mwanamke na Maendeleo wa Shirika hilo Edna Mtui, akizungumza na Walimu pamoja na Viongozi wa dini wa Kata hiyo wakati wa mafunzo hayo.
Afisa Elimu wa Shirika hilo John Nzungu, akizungumza na vijana kwenye mafunzo hayo
Afisa Maendeleo wa Shirika hilo Eliza Haji akizungumza na vijana kwenye mafunzo hayo. |
Mafunzo yakiendelea.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Shirika hilo, Hawa Hussein akizungumza na wazee na waganga wa jadi na Mangariba kwenye mafunzo hayo.
Mzee Omari Mbiaji, akichangia jambo kwenye mafunzo hayo
Mwalimu Mwanaidi Omari kutoka Shule ya Msingi Matumbo, akichangia jambo kwenye mafunzo hayo.
Mzee Ismail Njiru, akichangia jambo kwenye mafunzo hayo
Mwalimu Agnes Kiwale kutoka Shule ya Msingi Mkenge akichangia jambo kwenye mafunzo hayo. |
Wazee wakiwa kwenye mkutano huo.
Mzee Rajabu Mungi, akichangia jambo kwenye mafunzo hayo
Na Dotto Mwaibale, Singida
SHIRIKA la Empower Society Transform Lives (ESTL), limebaini kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia unachangiwa zaidi na mila potofu hivyo umetolewa wito kwa wananchi kuungana pamojakukabiliana na vitendo vyote vya ukatili kwa mtoto wa kike, hususan masuala ya ukeketaji na ukatili wa kijinsia ambayo bado hufanyika kwa siri sana kwa baadhi ya maeneo, hali inayohatarisha suala zima la ukuaji wa mtoto kiafya, kimwili, kiakili na kisaikolojia.
Akizungumza na wakunga wa jadi, wazee wa mila, mangariba, waganga wa jadi na wazee maarufu wa Kata ya Makuro wilayani Singida mkoani hapa jana, kwenye Mafunzo ya Ukatili wa Kijinsia, kupitia mradi wa ‘Tokomeza Ukeketaji Singida,’ unaofadhiliwa na Ubalozi wa Uholanzi, Afisa Miradi wa Shirika hilo, Annamaria Mashaka, alisema ukatili huo unachangiwa zaidi na mila na desturi kandamizi, ambazo zimeegemea zaidi kwenye dhana ya mfumo dume ndani ya jamii.
Mashaka alisema vitendo vya ukeketaji, mimba za utotoni, ndoa za utotoni na ndoa za kulazimishwa, usafirishaji wa binadamu imekuwa ni kama mtindo wa maisha kwa baadhi ya wazazi na walezi ndani ya kaya kwa kisingizio cha mila na desturi, hali inayopelekea madhara makubwa katika ukuaji wa mtoto na kuathiri maendeleo na utu wake.
Alisema uwepo wa mila na desturi potofu na matokeo hasi ya mfumo dume ni miongoni mwa sababu zinazochagiza kushamiri kwa vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia, huku wazazi na hasa wanaume ndani ya kaya kwa tamaa ya kupata utajiri wa haraka wakijikuta wanawaozesha mabinti zao walio katika umri mdogo, kwa kigezo cha kupatiwa mifugo au mali nyinginezo.
Mashaka alisema ndani ya mkoa wa Singida bado kuna changamoto kubwa ya idadi ya wanawake na watoto ambao wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa aina mbalimbali ikiwemo ukatili wa kingono, kimwili, kiuchumi na kisaikolojia huku takwimu za kitafiti zikionesha kuwa kati ya wanawake 100 ndani ya mkoa huo 31 wamekeketwa na wengi miongoni mwao wakijikuta tayari wamefanyiwa ukatili huo katika umri mdogo bila ya wao kujitambua.
Akichukua muda mrefu kufafanua dhana ya Jinsi na Jinsia, sambamba na mila nzuri na mila potofu, ikiwemo uwiano wa majukumu ya mwanaume na mwanamke ndani ya jamii katika muktadha wa dhana ya ukatili wa kijinsia na matokeo hasi ya mfumo dume, alisema jamii inapaswa kubadilika, ni wajibu wa kila mtu kwa nafasi yake kusimama na kukemea vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia.
Aidha, alisema pia ukatili wa kimwili mara kadhaa husababisha majeraha, ulemavu, matatizo ya kisaikolojia na hata vifo kwa akinamama na watoto.
“Ukatili wa kingono mathalani unaleta madhara makubwa katika afya ya mwanamke na mtoto wa kike kwa kusababisha mimba zisizotarajiwa, magonjwa ya
zinaa, kuharibu mifumo ya uzazi, Ukimwi,” alisema Mashaka na kuongeza; “Athari hizo ni kikwazo cha maendeleo ya mwanamke na mtoto wa kike katika kupata elimu, na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii,” alisema.
Afisa Mwezeshaji wa Mwanamke na Maendeleo wa shirika hilo Edna Mtui alisema makundi mengine yaliyokutanishwa kwa ajili ya kupata mafunzo hayo ni walimu, vijana na viongozi wa dini zote Wakristo na Waislamu ambao kwa pamoja wamesema ukeketaji na vitendo vyote vya ukatili sasa basi katika kata hiyo.
Alisema makundi hayo yameanzisha mpango mkakati wa kupambana na vitendo hivyo kwa ajili ya kuendelea kutoa elimu kuhusu ukatili huo makanisani, misikitini, mashuleni, kwenye
masoko, sehemu hatarishi na kwenye mikusanyiko ya watu.