Mkurugenzi Mkuu WA Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF ) Bernard Konga(kulia) na Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini Dkt Benson Ndiege (kushoto) wakisaini leo makubaliano ya kuwawezesha wakulima walioko ndani ya vyama vya ushirika nchini kujiunga na huduma za matibabu kupitia mpango wa bima ya afya.
Mkurugenzi Mkuu WA Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF ) Bernard Konga(kulia) na Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini Dkt Benson Ndiege (kushoto) wakionesha leo hati za makubaliano walizosaini za kuwawezesha wakulima walioko ndani ya vyama vya ushirika nchini kujiunga na huduma za matibabu kupitia mpango wa bima ya afya.
Mkurugenzi Mkuu WA Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF ) Bernard Konga(kulia) akiwa na viongozi mbalimbali wakionyesha hati za makubaliano walizosaini leo za kuwawesha wakulima walioko ndani ya vyama vya ushirika nchini kujiunga na huduma za matibabu kupitia mpango wa bima ya afya.
Mkurugenzi Mkuu WA Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF ) Bernard Konga(aliesimama) akitoa maelezo mafupi leo wakati wa hafla fupi ya kusaini makubaliano ya kuwawezesha wakulima walioko ndani ya vyama vya ushirika nchini kujiunga na huduma za matibabu kupitia mpango wa bima ya afya.
****************************
NA TIGANYA VINCENT
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika, umesaini makubaliano ya kuwawezesha wakulima walioko ndani ya vyama vya ushirika nchini kujiunga na huduma za matibabu kupitia mpango wa bima ya afya unaojulikana kama Ushirika Afya.
Makubaliano hayo yamesaini leo mjini Tabora kati ya Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga na Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini Dkt Benson Ndiege.
Konga alisema Ushirika Afya ni mpango maalum unaowezesha wakulima wa mazao mbalimbali, wafugaji walioko katika vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) kunufaika na huduma za bima ya afya kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Alisema kupitia mpango huu, mlengwa atatakiwa kuchangia kiasi cha shilingi 76,800 kwa mwaka na kuwa na fursa ya kupata huduma za matibabu kupitia mtandao mpana wa vituo vya kutolea huduma za matibabu zaidi ya 9,000 popote ndani ya Jumhuri ya Muungano wa Tanzania
Alisema kuwa hii ni fursa kubwa kwa wakulima kuweza kunufaika na huduma za matibabu kutokana na umoja wao kuwa chini ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika ambaye ndiye atakuwa mdamini Mkuu.
“Ushirkiano huu na makubaliano ambayo tunaingia hapa yanapanua wigo kwa kundi la wakulima kuweza kujiunga na kunufaika na huduma za matibabu, awali wakulima walikuwa wanakutana na changamoto ya kukosa fedha za mchango wa uanachama lakini kwa sasa Tume ya Maendeleo ya Ushirika itasimamia suala hili kwa kuwa mdhamini wa vyama hivi,” alisema .
Aliwahakikisha wakulima wote walioko kwenye vyama vya ushirika ambao watajiunga na huduma za Bima ya Afya kupitia mpango wa Ushirika Afya kunufaika na huduma bora na zenye uharaka zaidi wakati wowote watakapozihitaji.
Konga aliwaomba wakulima wote nchini kuhakikisha wanatumia fursa hii ambayo ni nafuu kwao kujihakikishia huduma za matibabu wakati wowote na hatimaye waweze kufanya shughuli zao za kilimo kwa uhakika zaidi bila kuuza mazao yao kwa lengo la kugharamia huduma za matibabu.
Alisema kuwa makubaliano ya ushirikiano huu unalenga kuongeza wigo wa wananchi na kuwapa uhakika zaidi wakulima wa kutekeleza majukumu yao.
Kwa upande wake Mrajis wa Vyma vya Ushirika, Dkt. Ndiege alisema kusainiwa kwa mpango huo ni faraa kubwa kwa wakulima na kuwajengea wananchi tabia ya kuwa ndani ya vyama vya ushirika ambako huduma mbalimbali zinapitia.
Alisema Mkulima ili aweze kufanya kilimo chenye tija ni lazima afya yake iwe njema na afya hii ataiona pale atakapokuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu pale anapopatwa na ugonjwa, hivyo kwa umuhimu huu tumeona ni vyema wakaingia makubaliano haya ambayo yana tija na maslahi makubwa kwa wakulima
Dkt. Ndiege alisema kuwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika itahakikisha pia inasimamia na kufuatilia huduma wanazopata ili fedha wanazolipa ziwe na tija katika afya zao.