Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani inayoongozwa na Mwenyekiti Dkt. Gervas Machimu (wa kwanza kushoto) ikikabidhi mahitaji mbalimbali ya kibinadamu kwa wauguzi wa Kituo cha Afya cha Halmashauri ya Manispaa ya Tabora Maili Tano wakati wa kuelekea kilele cha Maadhimisho ya siku ya Ushirika Duniani Julai 3,2021 yanayoendelea Mkoani Tabora
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika nchini Bi. Theresia Chitumbi (kushoto) pamoja na kamati ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani wakikabidhi mahitaji mbalimbali ya kibinadamu kwa Daktari Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora Kitete kwa ajili ya kuendeleza utoaji wa huduma bora hospitalini hapo.
……………………………………………………………….
Ushirika umetajwa kuwa nyenzo muhimu katika kuijali jamii na kuleta ushirikiano mzuri baina ya watu katika Jamii kwa malengo ya kuhakikisha jamii inauwa na mahusiano mema kwaajili ya kudumisha na ustawi wa Jamii na hatimaye kuleta matokeo chanya kiuchumi.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Bi. Theresia Chitumbi Julai 01, 2021 wakati akikabidhi mahitaji mbalimbali ya kibinaadamu katika Kituo cha Afya Maili Tano Halmashauri ya Manispaa ya Tabora akiwa ameambatana na kamati ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani mkoani Tabora.
Mwenyekiti Bi.Theresia ameeleza kuwa kujali Jamii ni miongoni mwa Misingi ya Kimataifa ya Ushirika ambapo kamati hiyo imetumia fursa ya maadhimisho ya Siku ya Ushirika ambayo imezinduliwa rasmi Juni 29, 2021 na kilele kufikiwa Julai, 03, 2021 kutekeleza msingi huo wa kujali Jamii. Kamati hiyo imekabidhi mahitaji ya kibinadamu mbalimbali yakiwemo Sabuni, Sukari, mafuta, miswaki, dawa za miswaki, taulo za kike vyenye thamani ya Shilling Millioni Mbili.
“Vyama vya Ushirika ni vina majukumu mengi ikiwemo Kujali Jamii kwani Ushirika unaundwa na Jamii hivyo kuleta mahitaji haya katika Kituo hiki cha Afya Maili Tano ni sehemu ya kutimiza wajibu na msingi wa Ushirika tumeona ni vyema kutekeleza hili hasa tunapoelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani,” alisema Bi. Theresia
Kamati ikikabidhi mahitaji hayo Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani Dkt. Gervas Machimu nae alieleza kuwa sambamba na makabidhiano hayo maadhimisho yanaendelea katika Viwanja vya Nanenane Ipuli mkoani Tabora. Akaongeza kuwa kuwa Kituo hicho cha Afya ni jirani na eneo la Uwanja hivyo kamati imetekeleza wajibu huo kwa kuzingatia jamii iliyopo jirani na eneo la Maadhimisho hayo.
Dkt. Machimu aliendelea kwa kutoa mwaliko kwa wananchi kutembelea mabanda ya maonesho ambapo wadau wengi wa Sekta ya Ushirika kutoka maeneo mbalimbali wameshiriki pamoja na shughuli nyingine zinazofanyika uwanjani hapo ikiwa ni pamoja na semina, makongamano, upimaji wa afya, ushauri wa masuala ya Kilimo, huduma za kisheria na huduma nyingine nyingi.
Akipokea mahitaji hayo kwa niaba ya Kituo hicho muuguzi Zaituni Ally ameishukuru kamati hiyo ya Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani na kupongeza hatua iliyochukuliwa kwani mahitaji hayo yanakwenda kusaidia kuongeza utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa wanaofika katika kituo hicho.
Katika hatua nyingine Kamati hiyo iliendelea na makabidhiano ya mahitaji ya kibinadamu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kitete mkoani Tabora ambapo Mwenyekiti wa Shirikisho Theresia Chitumbi pamoja na Kamati ya maandalizi walikabidhi mahitaji mbalimbali yakiwemo sabuni, mafuta, Sukari, miswaki, dawa za miswaki, taulo za kike vyenye thamani ya Shillingi Millioni moja na nusu.
Akipokea mahitaji hayo Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho Dkt. Mark Waziri ameishukuru Kamati ya Maandalizi kwa niaba ya wanaushirika na kutoa wito kwa wadau wa Ushirika kuendelea kushirikiana na Jamii katika kuboresha na kuendeleza huduma bora za Jamii zinazonguka maeneo yenye Shughuli za Ushirika kwani kufanya hivyo kunakuza uhusiano mwema na hatimaye kuongeza tija ya uchumi wa Jamii na Taifa.