Na Dotto Mwaibale,Singida.
SHIRIKA la Empower Society Transform Lives (ESTL)
linalojishughulisha na utoaji wa huduma ya uelimishaji jamii kuondokana na Ukatili wa
kijinsia, ikiwemo ukeketaji, na mila potofu katika Mkoa wa Singida kwa ufadhili
wa Ubalozi wa Uholanzi limewakutanisha kwa pamoja wajumbe wa kamati ya ulinzi wa
mwanamke na mtoto (MTAKUWWA) ngazi ya Kata kuangalia namna bora ya kupambana
na ukatili.
Wajumbe hao ambao ni viongozi kutoka idara mbalimbali za
serikali, Asasi za Kiraia,viongozi wa dini na wawakilishi wa makundi ya watu wenye ulemavu chini ya
mwenyekiti wake Afisa Mtendaji wa Kata wamekutana juzi kwenye kikao cha mafunzo ya kuwajengea uwezo na kujadili mbinu za
kukabiliana na ukatili Kata ya Msange katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida.
Akizungumza katika kikao hicho Afisa Miradi wa Shirika hilo
Annamaria Mashaka alisema baada ya kuzijengea uwezo kamati za Mtakuwwa ngazi
ya kata wanaamini zitakwenda kutekeleza mpango huo kupitia majukumu
yaliyoainishwa na mwongozo ambayo yamewekwa pia katika lugha rahisi na kamati hiyo ili
waendelee na mchakato wa kutokomeza ukatili kwa jamii ya watu wa Msange.
Alisema lengo la kuwajengea uwezo wajumbe wa kamati hiyo ni
kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ya mpango kazi wa Taifa wa
kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na mtoto ambao katika halmashauri hiyo unafanyika
katika Kata za Msange, Ikhanoda, Mudida na Mukuro.
” Miongoni mwa majukumu waliojipangia kama kamati katika
utekelezaji wa mpango huo ni kuendelea kutoa elimu, kuhamasisha jamii kuepukana na
vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto,” alisema Mashaka.
Aidha Mashaka alisema kamati hiyo ineelekeza nguvu katika
kuibua changamoto hama matukio yote yanayotokana na ukatili na si tu kuyaibua na
kufanya ufuatiliaji ili haki iweze kupatikana kwa wahanga wa ukatili na watuhumiwa waweze
kuhukumiwa kutokana na vitendo wanavyofanya.
Pia Mashaka alisema sambamba na kutoa elimu na kuibua matukio
kamati hiyo imewekeza nguvu katika kuhamasisha jamii kupitia mbinu
mbalimbali yakiwemo mabonanza ambayo yatafanywa kwa kushirikiana na Polisi Jamii
ngazi ya kata yakiwa na lengo la kutokomeza ukatili huo katika kata hiyo ya
Msange.
Afisa Mwezeshaji wa Mwanamke na Maendeleo wa shirika hilo Edna Mtui alisema wamekutana
na kamati hiyo kuongelea ukati huo na
aina tano ambazo zinawakumba sana wanawake na watoto wadogo ambao ni ukatili wa kingono, kimwili,
kisaikolojia, kiuchumi na ukatili wa kiafya.
Alisema wanakamati hao pia walitamani kujua je mtu
akifanyiwa ukatili sehemu husika ya kwenda kutoa taarifa ni wapi ambapo pia walipitia
vipengere mbalimbali ili kujua ni sehemu gani wataweza kulisema suala hilo la ukatili.
Alisema katika kata hiyo
bado kunaonesha kuna ukatili wa
ukeketaji ambao ni wa kiafya, kimwili na kingono ambao unafanyika kwa siri kubwa
sana ambapo wamegundua mbinu mpya kwa kufanya ukeketaji kwa mtoto mdogo
kuanzia anapozaliwa mpaka anapokuwa na miaka mtano.
Alisema ukatili huo wanaufanya kwa kutumia chumvi ya magadi,
mazinzi yanayotoka juu kwenye nyumba za tembe na kusugua sehemu za siri kwa
kutumia mtula ambapo pia mabibi wanafuga kucha ambazo hutumika kumfinya mtoto
kwenye kiungo chake ili kumkeketa jambo ambalo wamekiri kuwa ni baya.
Kamati hiyo imepanga mkakati wa muda wa miezi mitatu ili
kuendelea kutoa elimu kuhusu ukatili huo na kuwa wataitoa makanisani, misikitini,
mashuleni, kwenye masoko, sehemu hatarishi na kwenye mikusanyiko ya watu.
Mjumbe wa Kamati hiyo PC Christian kutoka Kituo cha Polisi
Kata ya Msange alisema matukio hayo ya ukatili ni muhimu yakatokomezwa na changamoto
kubwa iliyopo ni wahusika wa matukio hayo kushindwa kufika kwenye vyombo
vinavyotoa haki kutoa ushahidi jambo linalosabisha kesi hizo kuishia njiani bila kutotolewa hukumu.