Mchungaji wa Kanisa la Moravian Usharika wa Sabasaba mkoani hapa,Samuel Ngamanja akizungumza na waumini wa Kanisa hilo kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake wa kanisa hilo yaliyofanyika Jumapili ambapo alisema wanatarajia kufanya maombi maalumu kufuatia kuwepo kwa wimbi la tatu la ugonjwa wa virusi vya corona. Kulia ni Mtumishi wa Mungu Anna Emanuel na katikati ni muumini wa kanisa hilo, Beatrice Msai ambaye aliongoza ibada ya maadhimisho hayo.
Mchungaji Samuel Ngamanja akitoa baraka kwa waumini wa kanisa hilo baada ya kumalizika kwa ibada ya maadhimisho hayo.
Na Dotto Mwaibale, Singida
MCHUNGAJI Samuel Ngamanja wa Kanisa la Moravian Usharika wa Sabasaba mkoani hapa amewaomba waumini wa kanisa hilo yafanyike maombi maalumu kufuatia kuwepo kwa wimbi la tatu la ugonjwa wa virusi vya corona.
Ngamanja alitoa ombi hilo juzi wakati akizungumza na waumini hao kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake wa kanisa hilo yaliyofanyika Jumapili.
“Ndugu zangu niwaombe sana tunakila sababu ya kumuomba Mungu wetu atuepushe na janga ili la wimbi la tatu la ugonjwa wa virusi vya corona ambavyo tumeelezwa kuwa ni vibaya zaidi kuliko vyote vilivyotangulia wiki ijayo tutaandaa siku maalumu ya kufanya maombi hayo dhidi ya ugonjwa huo,”. alisema Ngamanja.
Ngamanja aliwaomba waumini hao kuendelea kuchukua tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa huo kama alivyoagiza Rais Samia Suluhu Hassan.
Mtumishi wa Mungu Anna Emanuel akihubiri katika maadhimisho hayo aliwataka wanawake kuwa na upendo kama aliokuwa nao Dorcas mwanamke aliyetajwa kwenye biblia ambaye alitumia muda wake wote kusaidia watu mbalimbali.
Emanuel aliwaomba wanawake hao kujenga tabia ya kuwa na matumizi mazuri ya fedha na akahimiza umuhimu wa utoaji wa sadaka.
“Sisi wanawake ni jeshi kubwa na ndio wasimamizi wa mambo yote katika nyumba tunapaswa kuwa na matumizi mazuri ya fedha tuache matumizi ya hovyo kwa kununua nguo wakati zingine zikiwazimejaa kwenye makabati hamjazifaa zaidi ya mwaka na vyakula vingi mlivyo vinunua vikiharibika kwenye majokofu yenu kwa kuhoza bila ya kutumika,” alisema Emanuel.
Pia alitumia nafasi hiyo ya mahubiri kuwaomba wanawake kuacha tabia ya kuwanyanyasa wanaume zao pale wanapokuwa hawana fedha kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya kutokuwa na kazi.
Wanawake wa kanisa hilo wanatarajia kuanzisha shughuli za ujasiriamali kwa lengo la kujipatia fedha zitakazo wasaidia kwa shughuli mbalimba sambamba na kuyasaidia makundi yenye uhitaji na tayari wamenunua sufuria kwa ajili ya upikaji wa vyakula.