****************
Na Ahmed.Mahmoud,Arusha
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini,IGP ,Simon Sirro amewataka wenyeviti wa serikali za mitaa,watendaji kata na vijiji kuwa macho kwa kuwatambua wageni wanaoingia katika maeneo yao ili kuepusha nchi kuingia kwenye matukio ya ugaidi na uhalifu.
Aidha ameagiza kata zenye changamoto za matukio ya uhalifu ,ubakaji,watoto kutelekezwa au matukio mengine zitapelekewa askari polisi ili kuweza kudhibiti matukio hayo.
Akizungumza jana Jijini Arusha na watendaji kata,wenyeviti wa serikali za mitaa,viongozi wa dini,polisi jamii pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali,IGP Sirro alisisitiza lazima wenyeviti hao wahakikishe amani na utulivu unakuwepo katika jamii
“Nasema hivi kwasababu hapa Arusha ni eneo hili limepakana na nchi jirani hivyo kuingia kwa wageni wasio na nia njema na nchi yetu ni rahisi hivyo ni lazima kila mmoja awe makini na wageni hao ili tusirudi miaka iliyopita ya mabomu katika maeneo mbalimbali”
Aliwataka viongozi hao kutanguliza maslahi ya Taifa na wananchi badala ya maslahi yao kwa kuwa mstari wa mbele kufichua wahalifu na uhalifu unaofanyika katika maeneo yao
Aidha Sirro alibainisha kuwa kata zenye changamoto mbalimbali ikiwepo kata ya Olasiti ili kukomesha matukio ya kiuhalifu yanayojitokeza ni vema kukawa na polisi kata kwaajili ya kutatua kwa haraka changamoto zinazowakabili wananchi wa eneo hilo
Pia aliagiza mikutano ya kila mwezi Kati ya Mkuu wa Polisi Wilaya(OCD) na viongozi wa ngazi mbalimbali za chini kwaajili ya kupeana taarifa za matukio mbalimbali na kuzitatua kwani uhalifu unaanzia majumbani,mitaani na maeneo mengine
“Tunahimiza ushirikiano na wananchi juu ya ulinzi shirikishi kwani bado polisi ni wachache ukilinganisha na watanzania waliopo hivyo ushirikiano ni muhimu katika kufichua na kukomesha matukio ya kiuhalifu”
Pia IGP Sirro aliwaonya wanaojiingiza katika matukio ya uhalifu na ugaidi kuacha mara moja kwani endapo watahusika katika katika uhalifu watashughulikiwa kama wahalifu wengine”
Akizungumza kuhusu madawa ya kulevya alisema Arusha ni Mkoa wa pili kwa uuzaji wa madawa ya kulevya hivyo ni aibu na lazima hatua zichukuliwe ili kudhibiti matukio hayo ambapo alisisitiza doria zitaimarishwa zaidi katika maeneo husika ili kudhibiti suala hilo la madawa ya kulevya haswa katika kata ya Ungalimited
Awali Mkuu wa Wilaya ya Arusha,Sophia Mjema alisisitiza umuhimu wa ulinzi na usalama ngazi za chini ni lazima ili kuleta maendeleo katika kila kata na serikali za mitaa
Wakati huo huo,Mbunge wa Arusha Mjini,Mrisho Gambo alisema Arusha ni Jiji la Utalii lakini huwezi kufanya utalii bila kuwa na amani usalama na kusisitiza lazima ulinzi uimarishwe.
Wakati huo.huo IGP Sirro ametoa sh, milioni 5 na Gambo sh, milioni 5 kwaajili ya ujenzi wa kituo cha Polisi cha Olasiti huku Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dk John Pima akiahidi kumalizia vituo vingine vya polisi kwaaajili kudhibiti matukio ya uhalifu.
Kata ya Olasiti ni miongoni mwa kata ndani ya jiji la Arusha zinazokabiliwa na matukio mengi ya kiuhalifu ikiwemo ubakaji wa watoto na wanawake pamoja na matukio mengine ya uhalifu