*********************
SHIRIKISHO la Sanaa za Ufundi Tanzania (TAFCA) limetangaza Kamati tano zitakazofanyakazi kama Wizara za Shirikisho hilo.
Akizungumza juzi baada ya uchaguzi Mkuu wa Shirikisho hilo uliofanyika kwenye ukumbi wa Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam, Rais wa TAFCA, Adrian Nyangamale alisema pamoja na Wizara hizo ameweka hadharani Jumuiya za shirikisho kwa malengo ya kutengeneza mifumo shirikishi kwa ajili ya kufanya kazi kama timu.
“Baada ya uchaguzi tumeazimia kutangaza Kamati tano na Jumuiya mbili ambazo zitasaidia kuliendesha Shirikisho, tunajipanga na Kamati ya utendaji kuteua watendaji wa nafasi hizo Saba,” alisema Nyangamale.
Aidha Nyangamale alizitaja kamati hizo tano ni Mipango, Uchumi na Fedha huku kamati nyingine ni Haki,Sheria na Katiba nyingine ni Elimu na Mafunzo ya Ufundi ujuzi.
Kamati nyingine ni Maendeleo ya Wanawake na Watoto na ya mwisho ni Habari, mahusiano na matukio huku kwa upande wa Jumuiya ni Umoja wa Wanawake wa TAFCA na Jumuiya ya wanafunzi wa Sanaa za Ufundi Tanzania.
Alitoa wito kwa viongozi wenzake kutekeleza majukumu ipasavyo ili kulisukuma mbele gurudumu la maendeleo.
Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni pamoja na Nyangamale (Rais), Makamu wake ni Rukia Walele wajumbe ni Linda Masholla, Safina Kimbokota, Abdallah Kiponda, Azimina Azimkhan, Rashid Mbago, Marco Tibasima na Mussa Sango ambao kila mmoja alichaguliwa kwa kura 30 za ndio.
Uchaguzi huo ulisimamiwa na baadhi ya watendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).