**********************************
Na Mathew Kwembe, Mtwara
Wanariadha Benedict Mathias wa Pwani na Thereza Bernard wa Simiyu wamejizolea medali za dhahabu katika mbio fupi za mita 200 na 400 zilizofanyika jana katika uwanja wa chuo cha ualimu Mtwara.
Katika fainali za mbio ndefu za mita 800 medali za dhahabu zilichukuliwa na wanariadha Damian Patrick wa Arusha na Loema Awaki wa Manyara.
Benedict ambaye ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Filbert Bayi ya Pwani alionyesha umahiri katika mbio za mita 100, 200, na 400 ambapo katika michuano yote hiyo alishinda.
Katika mbio za mita 100 Benedict alitumia sekunde 11:22, katika mbio za mita 200 alitumia sekunde 22:28 na katika mbio za mita 400 alitumia sekunde 49:97.
Kwa upande wa Thereza Bernard wa Simiyu, yeye alishiriki na kushinda mbio za mita 200, na 400 ambapo kwa upande wa mita 100 mshindi ni Bora Hassan wa Tabora.
Thereza alitumia sekunde 27:62 kushinda medali ya dhahabu katika fainali ya mbio za mita 200, na alitumia dakika 1:02:09 kushinda mbio za mita 400.
Mshindi wa pili kwa upande wa wavulana katika mbio za mita 200 ni Kassim Hamis wa Unguja ambaye alitumia sekunde 23:19 na nafasi ya tatu imeshikwa na mwanariadha Said Hamis pia wa Unguja aliyetumia sekunde 23:19.
Nafasi ya pili kwa wasichana mbio za mita 200 ilishikwa na Siwema Julius wa Pwani aliyetumia sekunde 28:00 na nafasi ya tatu ilichukuliwa na Bora Hassan aliyetumia sekunde 28:19.
Kwa upande wa mita 400 wavulana nafasi ya pili ilichukuliwa na Rahim Said wa Dodoma ambaye alitumia sekunde 53:50, na nafasi ya tatu ilikwenda kwa Manoni Mwigulu wa Geita ambaye alitumia sekunde 53:85 kukimbia mbio hizo.
Kwa wasichana mita 400 nafasi ya pili ilichukuliwa na Traifina Rajabu wa Singida ambaye alitumia dakika 1:02:72 na nafasi ya tatu ilikamatwa na Rebecca Kilipasi aliyetumia dakika 1:03:97.
Katika fainali za mbio za mita 800 medali ya dhahabu kwa wasichana ilitwaliwa na Loema Awaki wa Manyara ambaye alitumia dakika 2:21:03, nafasi ya pili ikichukuliwa naRahel Mila wa Simiyu aliyetumia dakika 2:21:97, na nafasi ya tatu ilishikwa na Rebeca Kilipasi wa Njombe aliyetumia dakika 2:22:25.
Wavulana mita 800 mshindi wa kwanza ni Damian Patrick wa Arusha ambaye alitumia dakika 1:59:38.nafasi ya pili ilichukuliwa na Jackson Charles wa Geita aliyetumia dakika 2:02:60 na nafasi ya tatu ilikwenda kwa Tiluli Machimani wa Morogoro ambaye alitumia dakika 2:02:63.
Wanariadha Loema Awaki na Damian Patrick wa Arusha pia wamekwishajizolea medali za dhahabu katika fainali za mbio za mita 1500, na 3000.
Katika fainali za mbio za kupokezana kijiti fainali ya mita 400 x 4 nafasi ya kwanza kwa wavulana ilishikwa na wanariadha wa Unguja, nafasi ya pili na ya tatu zilibebwa na wanariadha wa mikoa ya Pwani na Tabora.
Katika fainali ya mbio za kupokezana kijiti kwa wasichana nafasi ya kwanza ilichukuliwa na Tabora na mikoa ya Mara na Singida ilishika nafasi za pili na tatu.