Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe anayesomea Shahada ya Umahiri ya Sayansi Katika Mipango na Menejimenti ya Miradi, bwn.Nelson Kissanga akielezea ubunifu kisasa alioubuni wa ufugaji wa Samaki na kilimo cha mbogamboga kwa pamoja.
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Shahada ya Sayansi katika TEHAMA na Menejimenti Bi. Adelina Deusdedith (mwenye tisheti) akielezea mfumo alioubuni wa kufuatilia afya ya mama na mtoto wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua.
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Shahada ya Uhasibu na Fedha wa Ezekiel Wellia akielezea bidhaa aliyoibuni ya Chai Tiba.
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Shahada ya Ualimu katika Uchumi na Hesabu akionesha jinsi mradi wa ufuatiliaji , upatikanaji ubora na ufanisi wa vyanzo vya maji vijijini unavyofanya kazi.Mradi huo umelenga kuihudumia jamii.
Wafanyakazi na Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe wakiwa tayari kutoa huduma bora.
*********************
Maonesho ya Kimataifa ya 45 maarufu Sabasaba yameanza kushika kasi, huku wananchi wakipata huduma na fursa mbalimbali kwenye Banda la Chuo Kikuu Mzumbe.
Akizungumza na Waandishi wa Habari waliofika katika banda la Chuo Kikuu Mzumbe lililopo karibu na Jukwaa kuu mkabala na banda la Tantrade Ngorongoro Hall, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chuo hicho Bi. Rose Joseph amewakaribisha Wananchi wote kutembelea maonyesho hayo na hasa banda la chuo hicho kujionea shughuli zinazotekelezwa na Chuo, ambazo ni kutoa mafunzo, Utafiti, Ushauri wa Kitaalamu na Huduma kwa jamii.
“Tupo hapa kuwahudumia Wateja wote na tunafanya usajili wa papo kwa hapo kwa Wanafunzi wanaotarajia kujiunga na masomo kwa fani mbalimbali katika mwaka wa masomo 2021/2022, usajili huu unahusisha ngazi zote kuanzia cheti,astashahada,shahada za awali na shahada za uzamili” Alisisitiza
Aidha Bi. Rose ameongeza mbali na udahili, Chuo Kikuu Mzumbe pia kinatoa ushauri wa kisheria bure kwa wananchi wote watakaofika kutembelea maonesho hayo kwa kipindi chote cha maonesho, Pamoja na kuonesha wananchi shughuli mbalimbali zinazofanywa na wanafunzi kupitia bunifu mbalimbali mifumo, Sayansi na teknolojia Pamoja na ujasiriamali.
Maeneo mengine ni shughuli mbalimbali zinazofanywa na chuo kupitia miradi mbalimbali ya ufadhili iliyolenga kuihudumia Jamii.
Chuo Kikuu Mzumbe kinashiriki kwa mara nyingine maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya 45 yaliyoanza Juni 28 hadi Julai 13 mwaka huu katika viwanja vya kimataifa vya Mwl.Julius Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa jiji Dar es Salaam