Miongoni mwa wahudumu wa kujitolea mkoani Ruvuma waliopewa msaada wa baiskeli 15 kutoka kutoka shirika la SATFkupitia ubalozi wa Marekani.
Katikati ni Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema akikata utepe kuzindua baskeli 15 zilizotolewa na ubalozi wa Marekani kwa wahudumu wa kujitolea Mkoa wa Ruvuma.
Miongoni mwa wahudumu wa kujitolea mkoani Ruvuma waliopewa msaada wa baiskeli 15 kutoka kutoka shirika la SATFkupitia ubalozi wa Marekani.
****************
WAHUDUMU 15 wa kujitolea ngazi ya Jamii ambao wamekuwa wanafanyakazi ya kuwasaidia watoto wa kaya masikini 423 mkoani Ruvuma wamepewa msaada wa baiskeli ili kuwasaidia kutoa huduma kwa jamii.
Msaada huo umetolewa na Shirika la Social Action Trust Fund(SATF) kwa udhamini wa mfuko wa dharura wa Rais wa Marekani wa kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI(PEPFAR), kupitia mfuko wa Balozi wa Marekani nchini Tanzania.
Akitoa taarifa kwa Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Pololet Mgema katika hafla fupi iliyofanyika kwenye viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa mjini Songea ,Mwakilishi wa Mkurugenzi wa SATF Dkt.Sylivia Ruambo amesema jumla ya shilingi milioni 3.7 zimetumika kununua na kusafirisha baskeli hizo hadi Songea.
Dkt.Ruambo amebainisha kuwa SATF inatekeleza mradi wa tuwalinde watoto katika Halmashauri tatu za Mkoa wa Ruvuma ambazo amezitaja kuwa ni Madaba,Songea na Nyasa na kwamba mradi huo ni wa mwaka mmoja.
Mradi umelenga kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu kupata huduma za elimu,afya,ulinzi na haki za mtoto pamoja na kuziwezesha kaya masikini kujenga uwezo kiuchumi,alisisitiza Dkt.Ruambo.
Hata hivyo amesema,pamoja na shughuli nyingine,mradi huo uliwajengea uwezo wahudumu 15 wa kujitolea katika ngazi ya Kata ambao wamekuwa wanasaidia kuielimisha jamii kuhusu haki za mtoto na ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Amesema,mradi umeamua kuwanunulia basikeli wahudumu hao ili kuwarahisishia usafiri na kuwafikia walengwa majumbani kwao.
Akizungumza baada ya kuwakabidhi basikeli hizo,Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Pololet Mgema ametoa rai kwa wahudumu hao kuzitunza basikeli hizo na kuendelea kuwatumikia walengwa kama mradi ulivyoelekeza.
Natambua kazi yenu kwa sehemu kubwa ni ya kujitolea,hivyo nawaomba mtangulize mbele maslahi ya jamii ili kuweza kutimiza adhima ya kuwahudumia,alisisitiza Mgema.
Mgema amelishukuru Shirika la SATF na PEPFAR kupitia ubalozi wa Marekani kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya mkoani Ruvuma ambako wanatekeleza mradi wa Tuwalinde ambao unahudumia watoto 423.
Naye Mwakilishi wa Balozi wa Marekani Jeremy Divis amesisitiza kuwa wapo tayari kuendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania kutekeleza miradi mbalimbali yenye tija kwa jamii ukiwemo mradi wa tuwalinde ambao unatekelezwa pia mkoani Ruvuma.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Juni 30,2021