*************************
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango hii leo Juni 30, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na mwenyekiti wa kundi la maseneta wa kifaransa marafiki wa Tanzania Mheshimiwa RONAN DANTEC.
Mazungumzo hayo yamefanyika katika jengo la Bunge la Seneti Paris Nchini Ufaransa.
Seneta Dantec amezungumza na Makamu wa Rais juu ya umuhimu wa kuhifadhi mazingira lengo likiwa ni kupunguza hewa mkaa duniani. Pia ameshauri uwepo wa mfuko wa fidia kwa wale watakaothirika na masuala ya kuhifadhi na kulinda mazingira.
Makamu wa Rais Amesema amefurahishwa na namna uhifadhi wa mazingira unavyofanyika nchini ufaransa ikiwemo Mji wa Paris licha ya ukongwe wa mji huo. Amemuhakikishia Seneta Dantec kwamba Tanzania ipo tayari kushirikiana na Ufaransa katika uhifadhi wa mazingira na kuwakaribisha Maseneta rafiki wa Tanzania katika kutekeleza hilo kwa pamoja. Amesema Tanzania inazingatia uhifadhi wa mazingira lakini kwa kulinda haki za wananchi wakati wa utekelezaji wa uhifadhi huo.
Pia Makamu wa Rais ametembelea maktaba iliopo katika jengo hilo na kujionea historia mbalimbali iliohifadhiwa vizuri ya uongozi mbalimbali uliowahi kutawala Nchi ya Ufaransa.
Aidha Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ametembelea ukumbi wa Mikutano ya Bunge la Seneti na kupokea maelezo kutoka kwa Bi. Maryam Zadeh moja ya wahudumu katika Bunge hilo.
Makamu wa Rais yuko Nchini Ufaransa kuhudhuria Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa (Generation Equality Forum) linalofanyika Juni 30 hadi Julai 2 ,2021 lenye lengo la kuchagiza haki za usawa wa kijinsia kama zilivyokubaliwa katika mkutano wa Beijing wa mwaka 1995.