Serikali ya Marekani, kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), na Ng’wilabuzu Ndatwa Ludigija, Mkuu wa Wilaya ya Ilala wamekabidhi vifaa vya kuanzisha biashara vinavyoingiza kipato na samani za ofisini na vifaa vya kukusanya na kuhifadhi taarifa kwa wanufaika nchini. Ufadhili wa vifaa hutoa njia kwa vijana kustawi katika fani walizosomea kama vile ushonaji, useremala, uashi, uokaji, ufundi bomba, urembo wa nywele, upishi, na uandaaji wa chakula.
………………………………………………………………………
Serikali ya Marekani, kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), na Ng’wilabuzu Ndatwa Ludigija, Mkuu wa Wilaya ya Ilala wamekabidhi vifaa vya kuanzisha biashara vinavyoingiza kipato na samani za ofisini na vifaa vya kukusanya na kuhifadhi taarifa kwa wanufaika nchini.
Vifaa vya kuanzisha biashara vilitolewa kupitia mradi wa USAID wa Kizazi Kipya. Ufadhili wa vifaa hutoa njia kwa vijana kustawi katika fani walizosomea kama vile ushonaji, useremala, uashi, uokaji, ufundi bomba, urembo wa nywele, upishi, na uandaaji wa chakula. Kabla ya kupokea vifaa hivyo, Kizazi Kipya iliwasaidia vifaa vya kusomea na udhamini wa masomo kwa vijana kuhudhuria mafunzo ya ufundi katika vyuo vya mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), pamoja na vyuo vingine vilivyo na mamlaka ya kutoa mafunzo ya ustadi nchini Tanzania. Kwa jumla, Kizazi Kipya imesaidia vijana karibu 10,000 na udhamini wa ufundi na vifaa vya kuanzisha biashara kutoka halmashauri 81 katika mikoa 25 tangu mwaka 2018. Thamani ya jumla ya vifaa vya kuanzisha biashara vilivyokabidhiwa hadi sasa ni Shilingi za Kitanzania bilioni 15.2 (Dola za Marekani milioni 6.7).
Katika hafla hii, mradi wa ACHIEVE wa USAID pia ulikabidhi vifaa vya ofisini kwa OR-TAMISEMI ili waweze kutoa huduma bora kwa watoto yatima na watoto walio katika mazingira hatarishi. Vifaa hivi ni pamoja na kompyuta, printa, samani za ofisini, pikipiki na vifaa vingine vya ofisi. Thamani ya jumla ya bidhaa zitakazokabidhiwa ni takriban Tsh. 613,000,000 / = (zaidi ya Dola za Marekani 265,000). Wanufaika wa OR-TAMISEMI ni pamoja na Ofisi za Maendeleo ya Jamii katika ngazi za wilaya na kata katika mikoa 24. Mwaka huu, ACHIEVE itakuwa imenunua vifaa vya ofisi na vitendea kazi vyenye thamani ya jumla ya takriban Tsh. Bilioni 1.1 (zaidi ya Dola za Marekani 470,000).
Katika hafla ya makabidhiano leo, Mkurugenzi Mkazi wa USAID Andrew Karas alisema kuwa Serikali ya Marekani imefurahi kushirikiana na Serikali ya Tanzania kukabidhi vifaa hivi muhimu. “Sisi wa USAID tunaamini kwamba ikiwa vijana wa Kitanzania watapata ujuzi unaohitajika sana, wakianzisha vyanzo vya mapato, na kuweza kushiriki kikamilifu na kuongoza juhudi katika maisha ya kiraia, basi watakuwa wamewezeshwa kuwa wazalishaji na kushirikishwa kama raia,” alisema.
Mkurugenzi Mkazi aliendelea kusema kuwa, “Miradi yetu ya ACHIEVE na Kizazi Kipya inathibitisha jinsi Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) lilivyo dhamiria kuimarisha Serikali ya Tanzania, na pia kuwawezesha na kuwalinda vijana na kaya zao hasa walio katika mazingira hatarishi. USAID inajivunia kuwa sehemu ya uwezeshaji vijana na mabadiliko ya jamii kuelekea uchumi jumuishi zaidi na wenye nguvu wa viwanda.”