Mshindi wa kwanza wa mbio za mita 100 Bora Hassan wa Tabora kushoto, akifuatiwa kwa karibu na Stumai Msemwa wa Njombe na Shija Paulpo wa Pwani ambao walimaliza mbio hizo katika nafasi tatu za juu katika fainali ya mita 100 mashindano ya UMISSETA iliyofanyika leo asubuhi uwanja wa chuo cha ualimu Mtwara.
Washiriki wa fainali za mbio za mita 1500 kwa upande wa wavulana wakichuana leo asubuhi ambapo Damian Patrick kutoka Arusha aliibuka mshindi katika mbio hizo.
……………………………………………………………………
Na Mathew Kwembe, Mtwara
Wanariadha Benedicto Mathias wa Pwani na Bora Hassan wa Tabora wameibuka washindi katika fainali ya mbio za mita 100 zilizofanyika leo katika uwanja wa chuo cha ualimu Mtwara.
Benedicto mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Filbert Bayi alitumia sekunde 11:22 kumaliza mbio hizo, huku nafasi ya pili ikichukuliwa na mwanariadha Ally Bakari wa Dar es salaam ambaye alitumia sekunde 11:44 na Kassim Khamis wa Unguja alishika nafasi ya tatu baada ya kutumia sekunde 11:45 kumaliza mbio hizo.
Kwa upande wa wasichana, mshindi wa kwanza ambaye ni Bora Hassan wa Tabora alitumia sekunde 13:19, akifuatiwa kwa karibu na Stumai Msemwa wa Njombe ambaye alikimbia muda wa sekunde 13:28 na nafasi ya tatu ilichukuliwa na mwanariadha Shija Paulpo wa Pwani ambaye alimaliza mbio hizo akitumia sekunde 13:47.
Katika fainali za mbio za mita 1500, washindi ni Damian Patrick wa Arusha na Loema Awaki wa Manyara ambao jana pia waliibuka kuwa washindi wa mita 3000.
Damian alitumia dakika 4:07:16, akifuatiwa na Paul Ndege kutoka Mara aliyetumia dakika 4:11:06 na nafasi ya tatu ilichukuliwa na mwanariadha Augustino Leonard wa Manyara ambaye alitumia dakika 4:12:44.
Kwa upande wa wasichana nafasi ya kwanza ilikamatwa na Loema Awaki wa Manyara ambaye alitumia dakika 4:44:50, nafasi ya pili ilichukuliwa na Ester Martin ambaye pia anasoma shule ya sekondari ya Filbert Bayi baada ya kutumia dakika 4:46:80 na nafasi ya tatu ilichukuliwa na Nyanzobe Mbahi wa Mara aliyetumia dakika 4:49:66.
Katika fainali za mbio za kupokezana vijiti mita 100 x 4 mwanariadha Stumai Msemwa wa Njombe aliwaongoza wanariadha wenzake watatu kutoka mkoa huo kujitwalia medali za dhahabu baada ya kutumia jumla ya sekunde 55:66, huku nafasi ya pili ikichukuliwa na mkoa wa Mara na Tabora ikashika nafasi ya tatu.
Michezo mingine ya riadha hatua ya fainali itafanyika kesho ambapo mshindi wa mbio za mita 200, 400 na 800 pamoja na mbio za kupokezana vijiti mita 400 x 4 zinatarajiwa kuhitimishwa katika uwanja wa chuo cha ualimu Mtwara.
Matokeo ya michezo mingine iliyofanyika asubuhi hatua ya robo fainali kwa upande wa mpira wa wavu wasichana Mtwara imeifunga Tanga seti 3-0, Dar es salaam imeifunga Tabora seti 3-2, Mara imeifunga Simiyu seti 3-0 na Mbeya imeichapa Manyara seti 3-0.
Kwa upande wa mpira wa kikapu wavulana robo fainali Pemba imeifunga Iringa kwa pointi 45-25, Mwanza imeishindilia Rukwa pointi 88-17, Songwe imechapwa na Lindi 9-10 na Mara imefungwa na Njombe kwa pointi 34-38.
Kwa upande wa mpira wa kikapu wasichana Songwe imechapwa na Ruvuma 9-23, Dodoma imeifunga Lindi 22-12 na Tabora imeibugiza Iringa vikapu 62-12.
Kwa upande wa mchezo wa mpira wa mikono, timu zilizoingia nusu fainali kwa wavulana ni Unguja, Dar es salaam, Tabora, na Morogoro, na kwa wasichana timu zilizoingia hatua hiyo ni Morogoro, Geita, Ruvuma na Unguja.