Baadhi ya washiriki wa mkutano huo wakiwa katika picha ya pamoja katika mkutano huo uliofanyika mkoani Arusha (Happy Lazaro).
************************
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha.Wamiliki wa maabara binafsi ambazo hazijasaliwa (bubu) wametakiwa kusajili maabara zao kisheria ili kuboresha huduma hizo sambamba na kusimamia utekelezaji wa maswala ya ubora wa vipimo kwa wagonjwa.
Hayo yalisemwa na Kaimu Mganga mkuu wa mkoa wa Arusha,Vones Uisso wakati akizungumza katika mkutano wa uhamasishaji wa huduma za maabara kwa wamiliki mkoa wa Arusha.
Uisso alizitaka maabara hizo kuhakikisha wanasajiliwa kisheria ili kuzingatia miongozo ya wizara ya Afya kwani yoyote atakayekiuka taratibu hizo na miongozo watachukuliwa hatua za kisheria.
Alisema kuwa, kuna changamoto nyingi zinazosababishwa na wamiliki wengi ikiwemo kuajiri watu wasio na utalaamu pamoja na usajili kutoka kwenye Baraza la wataalamu wa maabara ,kutosajili maabara zao huku waliosajili kutolipia ada ya kila mwaka, kuanzisha maabara sehemu ambazo hazitakiwi kuwa na maabara pamoja na maduka ya dawa kufanya vipimo vya maabara.
“nawaombeni sana mkiwa kama wamiliki wa maabara binafsi za Afya kulazimika kuzingatia sheria na kanuni namba 10 ya mwaka 1997 na miongozo ya wizara ya Afya, maendeleo ya jamii,jinsia,wazee na watoto inayoongoza uanzishwaji na usimamiaji katika kutoa huduma bora za maabara binafsi za Afya ili wagonjwa wapate Tiba sahihi kwa wakati.”alisema Uisso.
Aidha aliagiza wamiliki wote wa maabara binafsi wenye madeni kote nchini kukamilisha ulipaji wa madeni yao kwa wakati bila kusubiri kufuatwa na bodi kwa wasiosajiliwa maabara zao(maabara bubu)wafuate taratibu za usajili maduka ya dawa kufanya vipimo vya maabara waache haraka kabla ya hatua kali kuchukuliwa .
Naye Msajili wa maabara binafsi Tanzania , Dominic Fwiling’afu alisema kuwa,lengo la mkutano huo ni kuleta mrejesho kwa kile walichoona kwenye maabara zao baada ya kufanya ukaguzi hivyo wameleta matokeo ya kile walichoona kwenye maabara zao na watatoa melekezo Cha kufanya ili kuboresha huduma za maabara.
Alisema kuwa, wanatoa elimu namna ya kusimamia maabara ambapo wataweka mikakati ili kuhakikisha huduma zinaenda vizuri ,kwani lazima kuzingatia usajili na viwango vya ubora ili watanzania waweze kupata huduma iliyo bora.
Alifafanua kuwa ,kwa sasa hivi hakuna usumbufu wowote katika kusajiliwa na wapo wazi pale wanapohitaji huduma kwani wanasimamia ubora,ambapo wanaanza mchakato wa kupeleka elimu katika ngazi ya kata na halmashauri ili endapo wataanzisha maabara ambayo hawaijui waweze kutoa taarifa ili ifanyiwe kazi kwa haraka zaidi.
Naye Meneja wa mamlaka ya dawa na vifaa tiba ( TMDA )Kanda ya kaskazini ,Proches Patrick alisema kuwa, wamekuwa wakifanya ukaguzi wa maabara ili kuhakikisha ubora ,usalama na ufanisi wa vifaa tiba vinavyotumika katika maabara zinazotoa huduma kwa wananchi ambapo kumekuwepo kwa baadhi ya maabara hizo kutumia vifaa tiba vya serikali ambavyo ni kosa na hairuhusiwi ambapo wahusika wameshachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.
Proches alitoa rai kwa wamiliki wa maabara kufuata sheria na taratibu kwani mali za serikali zinalengwa kwa ajili ya serikali na sio kutumika vinginevyo , hivyo aliwataka wadau hao kutumia vifaa tiba kutoka vyanzo sahihi lakini sio kutumia vifaa tiba vya serikali.