…………………………………………………………………………
Na Damian Kunambi, Njombe.
Wanachama wa UWT wilaya ya Ludewa mkoani Njombe wametakiwa kusimamia na kutekeleza mpango wa kujiimarisha kiuchumi sambamba na uhai wa chama katika kipindi cha miaka mitatu kilichopitishwa ili kuweza kukuza uchumi wao na chama kwa ujumla.
Hayo ameyasema katibu wa Chama cha mapinduzi (CCM) wilayani humo Bakari Mfaume katika mkutano wa baraza la kazi la UWT wilayani humo na kuongeza kuwa kamati ya siasa ya wilaya hiyo pamoja na kikao cha halmashauri kilipitisha mpango wa miaka mitatu wa chama kujiimarisha kiuchumi pamoja na kuimarisha uhai wa chama ambapo jumuiya za ngazi zote zinapaswa kufuata mpango huo.
Amesema chama hicho kina wanachama wanawake zaidi ya elfu kumi na saba kwa wilaya nzima lakini idadi hiyo ya wanachama haiwiani na takwimu zilizopo katika jumuiya hiyo ya lUWT kitu ambacho kinawapasa viongozi wa jumuiya hiyo kufanya juhudi za kuwahamasisha wanawake wenzao ili waweze kujiunga.
Ameongeza kuwa ili wanawake wengine waweze kupata hamasa ya kujiunga na jumuiya hiyo wanachama waliopo wanappaswa kuwa mfano wa kuigwa katika kujenga mahusiano yao pamoja kujijenga kiuchumi.
” Huwezi kumshawishi mtu ajiunge na jumuiya yenu wakati nyinyi wenyewe mliopo hamuelewani kila mnapolkutana mnagombana na kusengenyana badala ya kujadili masuala ya maendeleo hivi mkiishi katika mazingira hayo ya kugombana mnategemea nani atakuja kujiunga na jumuiya yenu?”, Alisema Mfaume.
Sambamba na hilo mfaume aliwataka wanachama wote wa jumuiya hiyo kuimarisha miradi mbalimbali iliyopo katika ngazi za kata ili waweze kuinuka kiuchumi na kuweza kujitegemea.
Katika kutambua juhudi hizo za kiuchumi kwa wanajumuiya hao katibu huyo aliwasilisha mchango wa fedha milioni mbili na laki sita kutoka kwa Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga kwa kushirikiana na mbunge wa viti maalum mkoa wa Njombe balozi Dk. Pindi Chana uliotolewa kwa lengo la kusapoti miradi mbalimbali ya jumuiya hiyo iliyopo katika ngazi ya kata.
” Fedha hizi zimeletwa ili zigawiwe kwa kata zote 26 na kusukuma miradi iliyopo ili iweze kupiga hatua zaidi na kuimarisha uchumi wa jumuiya hii na chama kwa ujumla hivyo nawaomba mkazitumie ipasavyo na kiasi hiki kikazae matunda mema ili hata wanaotuchangia wakaone mafanikio yetu”, Alisema Mfaume.
Leah Mbilinyi ni mwenyekiti wa UWT wilayani humo aliwashukuru wabunge hao sambamba na kuwataka wanachama wake kuwa makini katika uendeshwaji wa miradi iliyopo katika ngazi ya kata ili iweze kuwasaidia katika mahitaji mbalimbali ya kichama.
Aliongeza kuwa inapofanyika mikutano ngazi ya wilaya wanachama wamekuwa wakitarajia kulipwa nauli pamoja na posho kutoka kwa wahisani mbalimbali hivyo aliwataka viongozi wote wa ngazi ya kata kuikuza miradi hiyo ili iweze kuwawezesha kujitegemea wenyewe pasipo kutegemea wahisani.
“Hii miradi tunapoisimamia vyema itasaidia kuimega hata katika ngazi ya matawi hivyo wanawake wenzangu tuamkeni na tuimarishe miradi yetu kwani kwa kufanya hivyo itatuwezesha kusimama kwa miguu yetu wenyewe”, alisema Bi. Mbilinyi.