Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakifuatilia mada kuhusu bonde la Mto Kilombero katika kikao kilichofanyika mjini Morogoro jana.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akielezea kuhusu msimamo wa Serikali wa kukabiliana na uvamizi wa bonde la Mto Kilombero, kwenye kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kilichofanyika mjini Morogoro jana.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Angelina Mabula (Mb) akizungumza kuhusu msimamo wa Serikali juu ya mipaka ya ardhi ya vijiji vilivyo jirani na bonde la Kilombero wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kilichofanyika mjini Morogoro jana.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Martin Shigela akizungumza neno la utangulizi kwenye kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kilichofanyika mjini Morogoro jana.
Afisa Wanyamapori Mkuu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Pellage Kauzeni akiwasilisha mada kuhusu jitihada za Serikali za kusimamia bonde la Mto Kilombero katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kilichofanyika mjini Morogoro jana.
**************************
Serikali itaendelea kukabiliana na wavamizi katika bonde la Mto Kilombero ili kupunguza uharibifu unaotokana na shughuli za kibinadamu za kilimo na ufugaji zinazohatarisha maendeleo ya mradi wa bwawa la kufua umeme wa maji la Nyerere.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Wizara ya Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kilichofanyika mjini Morogoro leo.
“Wizara ya Maliasili na Utalii itahakikisha inapunguza uvamizi kwenye eneo la bonde la Mto Kilombero ili kuokoa kiini cha bonde hilo kinachotiririsha maji kwenye mradi wa bwawa la kufua umeme wa maji la Nyerere” Mhe. Masanja amesisitiza.
Amesema lengo la kuondoa uvamizi katika bonde hilo ni kutokana na umuhimu wake wa kuchangia asilimia 62 ya maji kwenye bwawa la Nyerere linalotarajiwa kuzalisha umeme wa megawati 2115 ambao pia utasaidia uendeshaji wa mradi wa reli ya kisasa SGR.
Ameongeza kuwa, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imetembelea eneo hilo ili kuangalia namna ya kuokoa kiini cha bonde hilo kinachotiririsha maji katika bwawa la Nyerere.
Aidha, Naibu Waziri Mary Masanja ameelezea kuwa Serikali imewahi kufanya doria ya kuondoa wavamizi ikiwa ni jitihada za kulitunza bonde hilo.
“Mwaka 2011 Serikali ilifanya doria ya kuwaondoa wakulima na wafugaji waliovamia eneo hilo lakini wananchi baadae wameendelea kusogea na kuchukua eneo la bonde ukubwa wa takribani square mita 4,400 kati ya square mita 6500 za bonde lote” Mhe. Masanja amesema.
Naye, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Angelina Mabula (Mb) amesema ofisi yake itahakikisha inabainisha mipaka ya bonde la mto Kilombero ili kukabiliana na changamoto zinazotokana na wananchi kuvamia bonde hilo.
“Sisi kama Wizara jukumu letu kubwa ni kuangalia namna bora ya kubainisha upya mipaka halisi ambayo mwananchi hatakiwi kuvuka na pia kuweka kingo ambazo mtu hatakiwi kuzisogelea ili kulinda rasilimali hiyo.” Mhe. Mabula amesema.
Ameweka bayana kuwa Serikali kupitia Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi itatoa elimu kwa vijiji jirani na bonde hilo ili vione umuhimu wa kulitunza.
“Tusipolilinda hili bonde halitaendelea kulisha mradi wa Mwalimu Nyerere kitu ambacho Serikali haipo tayari kitokee” Mhe. Mabula amesisitiza.
Pia, Dkt. Mabula amewaasa wananchi kuacha kulima katika bonde la Mto Kilombero.
“Hautakiwi kulima ndani ya bonde kwa sababu kadri unavyolima unaleta mmomonyoko wa udongo na kuharibu uoto wa asili na unakuwa umeua rasilimali hiyo yenye mchango mkubwa katika mradi wa bwawa la Nyerere” Dkt. Mabula amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Martine Shigela amesema ziara hiyo imemuwezesha kushuhudia uharibifu uliofanyika katika bonde hilo.
“Nimeshuhudia kuna nyumba zimejengwa karibu kabisa na mto na nimeona ng’ombe ambazo huoni mmiliki wake” amesema Mhe. Shigela.
Mhe. Shigela amewataka wafugaji kuhakikisha wanafanya shughuli zao za ufugaji katika eneo moja kwa lengo la kujiongezea kipato na pia kuchukua tahadhari ya kutambua uwezo wa mifugo yao na kilimo wanachokifanya ili bonde lifaidishe bwawa la Nyerere.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Dkt. Aloyce Kwezi (Mb) amesema ziara hiyo itaiwezesha kamati hiyo kuweka maoni vizuri kwa lengo la kumshauri Spika wa Bunge hatua za kuchukua.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, imehitimisha ziara ya siku mbili ambapo siku ya kwanza imelikagua bonde la Mto Kilombero lililovamiwa na wananchi wanaoishi karibu na bonde hilo.