Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MBUNGE
wa Dodoma Mjini, Mhe. Anthony Mavunde amewahamasisha watumishi wa Kituo cha
afya Makole kuchangamkia fursa ya kununua nyumba na viwanja vya makazi, katika
mpango unaoendeshwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF)
na Benki ya Azania.
Mhe.
Mavunde alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dodoma alipokuwa akipokea vifaa
tiba vilivyotolewa na PSSSF kwa Kituo cha afya Makole kama sehemu ya
maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa umma iliyoadhimishwa kuanzia Juni 16 hadi
23, 2021.
“Ndugu
wafanyakazi wa kituo cha Makole, nawahamasisha jitokezeni kutumia fursa hii ya
kumiliki nyumba na viwanja kama walivyosema wenzetu wa PSSSF, kwa mpango huu wa
kulipa kidogo kidogo, naamini kila anaweza kupata anachotaka, hivyo jitokezeni”
alisisitiza Mhe. Mavunde.
PSSSF
kwa kushirikiana na Benki ya Azania wana utaratibu wa kukopesha nyumba
zilizojengwa na Mfuko na viwanja kwa Wanachama wake na Wananchi kwa ujumla kwa
riba nafuu na masharti rafiki zaidi kwenye soko. Lengo la mpango huo ni
kuwawezesha wanachama na wananchi kumiliki nyumba na viwanja kwa utaratibu wa
kulipa kidogo kidogo kwa riba nafuu ya asilimia 10.Bei ya nyumba ni kati ya
millioni 36 hadi 61 kutegemeana na ukubwa wa nyumba.
Nyumba
zinazouzwa zipo katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Shinyanga, Tabora,
Mtwara na Iringa. Viwanja vipo Ruvuma, Kagera, Tabora, Iringa, Katavi,
Morogoro, Dar es Salaam, Rukwa, Lindi na Mtwara.
Akizungumzia
ziara ya PSSSF katika kituo cha afya Makole, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA.
Hosea Kashimba alisema, “Kwa kuzingatia ujirani wetu huu, PSSSF imekuwa ikitoa
misaada mbalimbali kwa kituo hiki ikilenga kuboresha huduma zitolewazo, kwani
kama mjuavyo nia ya serikali ni kuhakikisha kila mtanzania anapata huduma bora
za afya. Ili kuhakikisha tunaendeleza azma hiyo, katika maadhimisho ya Wiki ya
Utumishi wa Umma mwaka huu, tunachangia vifaa tiba katika kitengo cha kina Mama
Wajawazito na kitengo cha Meno kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma za tiba
ya meno ikiwemo utengenezaji wa meno bandia”.
Kwa
upande wa Mbunge wa Dodoma Mjini aliishukuru PSSSF kwa kuendelea kusaidia kituo
hicho ambacho alisema kwa sasa kinatoa huduma kwa watu wengi zaidi wakiwemo
watumishi wa PSSSF, na aliongoza, “Msaada huu utakwenda kuleta matokeo chanya
kwa wananchi wote.Pia Mkurugenzi Mkuu, naomba mkifanye kituo hiki kiwe rafiki
kwenu kwa kuendelea kutoa misaad mara kwa mara.
Mkurugenzi
Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), CPA Hosea
Kashimba (kulia) akikabidhi vifaa tiba kwa Mbunge wa jimbo la Dodoma (mjini).,
Mhe. Anthony Mavunde (katikati) na Kaimu Mganga Mfawidhi wa kituo cha afya cha Makole Bibi Tumaini Kapungu mwishoni
mwa wiki iliyopita. PSSSF imetoa msada huo kwa Kituo hicho kama sehemu ya
maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa umma iliyoadhimishwa kuanzia Juni 16 hadi
23, 2021.