Na Dotto Mwaibale, Singida
KAIMU Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani amewataka Maafisa Maendeleo ngazi za Halmshauri na Kata kuwasaidia vijana kuwaweka pamoja na kuunda vikundi.
Ndahani alitoa ombi hilo juzi wakati akikagua mradi wa kilimo wa vijana ujulikanao kwa jina la Singida Youth Agricultural Group uliopo Uhamaka Manispaa ya Singida.
Vijana hao kupitia mradi huo wanajishughulisha na kilimo cha matunda,mboga, ufugaji wa kuku na samaki.
Ndahani alisema asilimia 10 ya mkopo unaotolewa na halmashauri kwa ajili ya vijana hauwahusu vijana wa mjini pekee bali ni kwa kila kijana mwenye sifa aliyopo hata kijijini na wanatakiwa kupewa bila ya ubaguzi wowote.
” Jambo linalo nisikitisha kwenu licha ya kuwa na mradi mzuri na wenye tija hamjui kabisa namna ya kusajili vikundi na fursa za kupata mikopo kutoka halmshauri na Taasisi za fedha,” alisema Ndahani.
Hivyo aliwaomba maafisa vijana wenzake katika ngazi za halmshauri na maafisa maendeleo wa kata kuwasaidia kuwafundisha michakato yote ya kuanzisha vikundi ,kusajili na namna ya kupata mikopo.
Pia Ndahani aliwataka vijana wanao nufaika na mkopo huo kujenga tabia ya kurejesha haraka fedha hizo ili kutoa fursa kwa vijana wengine kukopeshwa.
Aliwahimiza vijana hao kujikita zaidi katika kilimo cha pilipili ‘maarufu mwendo kasi’ ambazo soko lake ni kubwa hapa nchini na nje ya nchi ambapo wilaya ya Kahama mkoani Geita ndio ni kinara wa kilimo cha zao hilo.
Mwenyekiti wa kikundi hicho Ally Hamisi ametoa shukurani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha upendo na imani kubwa kwa vijana wa makundi yote na hilo lilidhihirika wakati alipokuwa akizungumza nao jijini Mwanza ambapo alisisitiza kuendelea kuwapatia nafasi za uongozi na kuwawezesha kiuchumi.
Naye Katibu wa kikundi hicho Gwanaka Mwakyusa amemshukuru Kaimu Afisa Maendeleo Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani kwa kazi anayoifanya ya kuwaunga mkono vijana na moyo wa kipekee wa kuwasaidia akitolea mfano alivyo tumia muda mrefu kuwafundisha namna ya kusajili kikundi na jinsi ya kupata mkopo katika Halmshauri na kubwa zaidi anavyotumia gari lake kuwafikia vijana bila kujali gharama.
Naye Diana Gibson amewaomba vijana kujishughukisha na kilimo ambacho kimekuwa mkombozi kwa kwani kwa muda mrefu alikuwa akifanya kazi katika salooni mbalimbali lakini kipato alichokuwa akikipata kilikuwa ni kidogo ukilinganisha na anacho kipata sasa kupitia kilimo.