Mwanariadha Salma Charles (15) mwanafunzi wa darasa la saba wa shule ya msingi Nyaronyo, wilayani Ushetu akimaliza kukimbia mbio za mita 1500 leo asubuhi, huku akifuatiwa kwa mbali na aliyeshika nafasi ya kwanza katika mashindano ya riadha UMISSETA hatua ya robo fainali Loema Itimay wa Manyara.
Mwanariadha Salma Charles (15) akisindikizwa na Mwalimu wake Neema Chongolo mara baada ya kumaliza mbio za mita 1500 za UMISSETA leo asubuhi na kufanikiwa kuwa wa kwanza katika mbio hizo ambazo kwake ilikuwa ni maandalizi ya kushiriki mbio za riadha za kimataifa nchini Serbia
Mshindi wa kwanza wa kurusha tufe Abdallah Salum wa Unguja leo akijiandaa kurusha kisahani katika mchezo uliochezwa leo asubuhi katika uwanja wa chuo cha ualimu Mtwara.
…………………………………………………….
Na Mathew Kwembe, Mtwara
Mwanariadha Salma Charles Samwel wa Ushetu Kahama ambaye ni miongoni mwa wanafunzi 10 waliochaguliwa kujiandaa kushiriki mashindano ya kimataifa ya riadha huko Belgrade Serbia amedhihirisha ubora wake leo pale alipokimbia na wanariadha wanaoshiriki mbio za UMISSETA katika hatua ya robo fainali na kuwa wa kwanza
Salma ambaye alitamba katika mbio za mita 800 na mita 1500 kwenye michezo ya UMITASHUMTA iliyomalizika hivi karibuni, leo alikimbia mbio za mita 1500 na kutumia dakika 4:46:13 huku akimwacha aliyeshika nafasi ya kwanza kwa wanafunzi wa sekondari Loema Itimay wa Manyara ambaye alikimbia mbio hizo akitumia dakika 4:52:41.
Akizungumzia kiwango cha mwanariadha huyo, Mratibu wa riadha wa UMITASHUMTA na UMISSETA Robert Kalyahe amesema Salma na wenzake 9 wanaendelea vizuri na mazoezi kwa ajili ya kushiriki mashindano hayo ya kimataifa.
Amesema kwa vile wanafunzi hao 10 wapo kambini Mtwara ameona ni vyema awashindanishe na wanafunzi wa sekondari ili aweze kuona hatua waliyoipiga tangu kuanza kwa mazoezi yao.
Kalyahe anaamini wanariadha 6 watakaoshiriki mashindano ya kimataifa watafanya vizuri kulingana na program ya mazoezi wanayowapa wanariadha hao.
Mbali na Salma, mwanafunzi mwingine aliyeshiriki mbio za mita 1500 za UMISSETA hatua ya robo fainali ni Mwanaharabu Ally wa shule ya msingi Mtua wilayani Nachingwea ambaye alifanikiwa kushika nafasi ya tatu katika kundi lake.
Naye mwanafunzi Damian Christian ambaye anasoma kidato cha pili katika shule ya sekondari ya St Patrick ya Arusha alitia fora kwenye mbio hizo za mita 1500 baada ya kuwaacha mbali wanafunzi wenzake.
Damian ambaye ni mara yake ya kwanza kushiriki UMISSETA mwaka huu ameonyesha umahiri mkubwa katika kukimbia mbio ndefu na anatamani kufikia rekodi ya wakimbiaji wa zamani wa kimataifa wa Tanzania kama Filbert Bayi na Juma Ikangaa.
Mchezo wa riadha ambao leo umeingia siku ya pili utaendelea kuchezwa kwa siku tano mfululizo ambapo baadhi ya michezo ipo ngazi ya hatua ya nusu fainali na fainali.
Katika mchezo wa kuruka miruko mitatu aliyeshinda kwa upande wa wanariadha wasichana ni Witnes Ibrahim wa Geita aliyeruka umbali wa mita 9:87 na kufuatiwa na Mwalu Madirisha wa Tabora aliyeruka umbali wa mita 9:62 na nafasi ya tatu ilichukuliwa na Eugenia Simon ambaye aliruka umbali wa mita 9.36.
Mchezo wa miruko mitatu kwa wavulana mshindi ni Mussa Yusuph wa Shinyanga ambaye aliruka umbali wa mita 13:10, nafasi ya pili ilichukuliwa na Ewald Emanuel wa Manyara aliyeruka umbali wa mita 12: 90 na nafasi ya tatu imechukuliwa na Alphonce David wa Tabora ambaye aliruka umbali wa mita 12:60.
Kwa upande wa mchezo wa kurusha tufe wavulana mshindi wa kwanza ni Abdallah Salum wa Unguja ambaye alirusha umbali wa mita 14:30, nafasi ya pili ilichukuliwa na Edward Michael wa Dar aliyerusha tufe umbali wa mita 11:97, na nafasi ya tatu ilichukuliwa na Rajab Mtonyi wa Dodoma ambaye alirusha umbali wa mita 11:42.
Mshindi wa mchezo wa kurusha tufe kwa wasichana anaitwa Keflonia Daudi wa Shinyanga kwa umbali wa mita 8:93, nafasi ya pili ilichukuliwa na Martha Matinga wa Simiyu kwa umbali wa mita 8:88 na nafasi ya tatu ilikamatwa na Fatma Ussi Said wa Unguja kwa umbali wa mita 8:70