Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo (wa pili kulia), akipata ufafanuzi wa namna wanavyozalisha Marumaru kwa Mkurugenzi wa kiwanda cha Keda Ceramic Limited Bwa. Bruce ni, kiwanda kilichopo Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo (wa pili kushoto), akikagua mfumo wa maji taka katika kiwanda cha Keda Ceramic Limited kilichopo Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo (wa pili kushoto), akiwa katika ziara ya ukaguzi wa mazingira kiwanda cha H & J kinachozalisha mifuko ya viroba kilichopo Chalinze Mkoa wa Pwani.
******************
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo, amefanya ziara ya kushtukizia katika kiwanda cha H & J Limited kinachozalisha mifuko ya viroba kilichopo Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani.
Mhe. Jafo akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa Mazingira katika kiwanda hicho amebaini changamoto mbalimbali za kimazingira ikiwemo utiririshwaji wa maji machafu kutoka kiwandani hapo na kwenda kwenye Mto Mbiki uliopo karibu na kiwanda hicho.
Amesema changamoto nyingine ni uchomaji wa mifuko inayotumia malighafi ya plastiki pamoja na wafanyakazi wa kiwanda hicho kutokuwa na vifaa vya kufanyia kazi.
Aidha Mhe. Jafo amewataka wenye kiwanda hicho kurekebisha mara moja changamoto hizo ili kuepusha uchafuzi wa mazingira. Ameendellea kusema kuwa hayupo tayari kukifumbia macho kiwanda chochote kitakachohusika na uchafuzi wa mazingira kwani Serikali inataka maendeleo yenye tija na yanayohifadhi mazingira.
“sijaridhika na kiwanda hiki kinavyoendeshwa kwani kinachangamoto nyingi ikiwemo utiririshwaji wa maji kutoka kiwandani na kwenda kwenye mto mbiki, hivyo niwatake NEMC kuja hapa na kufanya ukaguzi pamoja na kuchukua hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria ya mazingira. Pia natoa miezi sita kwa kiwanda hiki kuweka mfumo wa uchujaji maji yanayotoka kiwandani kabla ya kwenda kwenye mazingira”. Amesema Mhe. Jafo
Kwa Upande wake Meneja wa Kanda ya Mashariki Kaskazini Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Bw. Anorld Mapinduzi, amesema kuwa kiwanda cha H& J kilisajiliwa kwa ajili ya kupata cheti cha mazingira lakini mchakato wa upatikanaji wa cheti haujakamilika na kiwanda kimeanza kufanya shughuli zake.
“Tumepokea maelekezo ya Mhe. Waziri na tutakuja kufanya ukaguzi wa kina ili tuweze kuwachukulia hatua kulingana na sheria na kanuni ya Mazingira. Ikiwa NEMC imepewa mamlaka ya kusimamia mazingira hatupo tayari kuona wananchi wanaathirika kwa moshi, vumbi au kemikali zozote zile.” Arnold Mapinduzi.
Vile vile Mhe. Jafo amekagua kiwanda cha Keda Ceramic Limited kilichopo Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani kinachojihusisha na uzalishaji wa marumaru, amekipongeza kiwanda hicho kwa jinsi wanavyofanya shughuli zao bila ya kuchafua mazingira na amewaomba wenye viwanda kuhakikisha wanafanya kazi zao bila ya kuathiri mazingira yetu.
Mhe. Jafo amefanya ziara katika Mkoa wa Pwani kwa kukagua utunzaji wa mazingira katika viwanda alivyotembelea.