Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, RAS Zuwena Omary Jiri akiwa na mumewe baada ya kukabidhiwa tuzo na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere, kama ishara ya zawadi ya utumishi uliotukuka kwenye nafasi ya Katibu Tawala wa Wilaya DAS Simanjiro iliyotolewa na Chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara, (MAREMA) Tawi la Mirerani.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere, akimkabidhi tuzo Katibu Tawala wa Mkoa RAS Shinyanga, Zuwena Omary Jiri kama ishara ya zawadi ya utumishi uliotukuka kwenye nafasi ya Katibu Tawala wa Wilaya DAS Simanjiro iliyotolewa na Chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara, (MAREMA) Tawi la Mirerani.
****************************
Na Gift Thadey, Simanjiro
KATIBU Tawala RAS wa Mkoa wa Shinyanga Zuwena Omary Jiri ambaye ameapishwa hivi karibuni jijini Dodoma na Rais Samia Suluhu Hassan amewaaga wananchi na viongozi wa Wilaya ya Simanjiro kwa kumuomba Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere, kusimamia uanzishwaji wa soko la madini.
Zuwena ambaye alikuwa Katibu Tawala DAS wa Wilaya ya Simanjiro na kuteuliwa kuwa Rais Samia kuwa RAS Shinyanga alitoa ombi hilo mji mdogo wa Mirerani, alipoagwa na kukabidhiwa tuzo ya utumishi uliotukuka na chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara (MAREMA) Tawi la Mirerani.
Amemuomba Makongoro afanikishe uanzishwaji wa soko la madini ya vito kwani jengo litakalotumika kwa uuzaji na ununuzi wa madini hayo ya vito lipo na limekamilishwa ujenzi wake.
Amesema ana imani mkuu huyo mpya wa mkoa wa Manyara, ataweza kutekeleza suala hilo la uanzishwaji wa soko hilo la madini ya vito ambalo lilikuwa lipo tayari kuanza.
“Mmiliki wa jengo hilo tulikubaliana naye kuwa akimaliza ukarabati wa ujenzi wa jengo lake, mchakato wa soko utaanza mara moja ila hadi hivi sasa imeshindikana ili hali jengo lipo tayari,” amesema Zuwena.
Amesema changamoto ya wafanyabiashara wa madini ambao ni wanunuzi wakubwa wa madini kuanzisha ofisi kwenye mji mdogo wa Mirerani ilikuwa kikwazo cha uanzishwaji wa soko hilo.
Hata hivyo, Makongoro amesema atapambana kuhakikisha soko hilo linaanzishwa japokuwa changamoto ya kutoa leseni ya wafanyabiashara wanunuzi wa madini kati ya mkoa wa Manyara na Arusha.
“Bado hakujapatikana muafaka wa eneo la kutolewa kwa leseni kwa wafanyabiashara wa wanunuzi wa madini ya Tanzanite kati ya mkoa wa Arusha au Manyara,” amesema.
Amesema leseni hizo ambazo hutolewa na ofisi ya madini ya mkoa bado hakujafikiwa muafaka rasmi hivyo inapaswa wachague leseni zitolewe Manyara au Arusha ili soko hilo lianze kazi.
Amesema hivi karibuni anatarajia kuanza ziara yake ya siku tano kwenye wilaya ya Simanjiro hivyo atakutana na wadau hao wa madini ili wakae pamoja na kujadili suala hilo kwa mapana yake.
MWISHO