KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo,akizungumza wakati akifungua Mkutano wa Baraza Kuu la UWT Taifa,uliofanyika leo Jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) Taifa ,Gaudensia Kabaka,akizungumza katika Mkutano wa Baraza Kuu la UWT Taifa,uliofanyika leo Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu UWT Queen Mlonzi,akizungumza katika Mkutano wa Baraza Kuu la UWT Taifa,uliofanyika leo Jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki wakifatilia hotuba ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo,(hayupo pichani) wakati akifungua Mkutano wa Baraza Kuu la UWT Taifa,uliofanyika leo Jijini Dodoma.
KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua Mkutano wa Baraza Kuu la UWT Taifa,uliofanyika leo Jijini Dodoma.
……………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo ameagiza kuanzia sasa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) liwe na agenda ya kudumu ya matumizi ya fedha asilimia 4 za wanawake zinazotolewa katika Halmashauri.
Ametaka Baraza hilo lijue Nchi nzima fedha kiasi gani zimetengwa, zimetolewa kwa kina mama wangapi kwani anazotaarifa kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wakijinufaisha na fedha hizo.
Akizungumza leo June 26,2021 wakati akifungua Mkutano wa Baraza Kuu la UWT Taifa,Katibu Mkuu huyo amesema matarajio ya chama ni kuona viongozi wanakuwa na agenda zenye mashiko katika jamii huku akihoji ni kwanini Baraza la mwaka huu halina agenda ya matumizi ya fedha asilimia 4 zinazotolewa katika Halmashauri.
“Kuanzia sasa agenda ya kudumu ya Baraza kuu la Jumuiya iwe matumizi ya fedha asilimia 4 za wanawake zinazotolewa katika halmashauri.Tujue nchi nzima fedha kiasi gani zimetengwa,zimetolewa kwa akina mama wangapi na kina mama wangapi wamenufaika sababu kina mama wengine ndio kina sie wengine wanatengeneza miradi ya kuwanufaisha ninyi,sisi kama chama hatupo tayari hili litokee,”amesema.
Amesema Baraza hilo ndio furum ya kuwazungumzia wanawake kuhusiana na fedha hizo ambapo amedai Halmashauri ya Kinondoni pekee imetenga shilingi bilioni 4 ambapo amehoji ni kwanini mwanamke alalamike suala la mtaji.
“Kwa sababu hii ndio forum ya kutengeneza mfumo sahihi msiwaache kina mama wenzetu mimi nimetoka Kinondoni mwaka huu wametenga bilioni 4 kwanini wanawake walalamike changamoto ya mitaji,”amesema.
Vilevile,amewataka Wabunge wanaotokana na UWT kuzisimamia na kuwa na taarifa ya asilimia 4 ya fedha zinazotolewa katika Halmashauri kwamba zinawanufaisha wanawake.
VIKAO
Aidha,Katibu Mkuu huyo ameitaka UWT kutumia vikao kuwasaidia wanawake na sio kuvitumia kusengenyana na mambo yao binafsi.
Amesema kwa sasa ukiona idadi ya wajumbe kwenye vikao imekamilika ujue kuna mtu anataka kushughulikiwa ambapo amedai jambo hilo sio zuri.
“Uhai wa chama ni vikao ni muhimu kwani ndio sehemu ya kujadili mambo yetu na uzoefu unaonesha vikao vyetu vingi vinakosa tija.Nasema kwa sababu tumekuwa na vikao kuanzia kamati ya utekelezaji,baraza kuu na vikao vingine vya juu muda mwingi sana katika vikao hivi ukiona ‘Colum’ imetimia na wajumbe wamefika ujue kuna mtu wanataka kumshughulikia.
“Vikao hivi vinafanyika ndani ya Jumuiya katika chama ambacho kimepewa nafasi ya kuongoza Nchi na kazi ya kuongoza Nchi sio kazi ya lelemama alisema Mwalimu Nyerere(Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) na sisi ndio tunatoa kazi ya uongozi sisi ni lazima tuwe mwarobaini wa kule tunapotoka.
“Kuna kina mama kila eneo sasa wanatakiwa wakuone wewe kama daraja vikao ndio vinatakiwa kuwa sehemu mahasusi sisi tumebahatika kuwemo katika vikao.Sisi tunawajibu wa kuheshimu msihangaike na mambo ya watu hangaikeni na mambo ya maendeleo UWT isiwe kwenda kujadili huyu mrefu ama mfupi jadilini mambo ya maendeleo tuwe ni viongozi ambao tunajitengenezea daraja uongozi usiwe ni kujadili sisi kwa sisi tujadili inshu,”amesema.
YEYE NI MKALI
Katibu huyo amesema yeye ni mgeni machoni mwa watu lakini anauzoefu wa zaidi ya miaka 20 na ameingia katika vikao muhimu vya chama hicho ambapo amedai yeye atasimamia taratibu ili kujenga maadili ndani ya chama.
“Niwaambie ninavyoongea nacheka hivi lakini mimi ni bingwa wa kusimamia taratibu ni lazima tujenge maadili kwenye chama chetu na lazima tusimamie hili na tuheshimu kwa dhati.
“Mimi ni Katibu Mkuu mpya ila mwenye kwao wanamjua niseme kweli mimi ni mgeni machoni mwa wengi lakini huu ukumbi nimeingia zaidi ya miaka 20 na nimebahatika kweli kuwa kijana mdogo ambaye nimeingia katika vikao muhimu vya Sekretarieti,Kamati Kuu,Maadili Taifa wakati ule nilikuwa Afsa lakini nimekuja kuwa Mkuu wa Maafsa,”amesema.
KUONEKANA WAKATI WA UCHAGUZI TU
Katibu Mkuu huyo amesema wanawake ni jeshi kubwa lakini limekuwa likionekana wakati wa uchaguzi tu hivyo amelitaka kujitokeza wakati wote kukipambania chama.
“Wanawake ni Jeshi kubwa lakini halionekani katika shughuli za kawaida ninyi mmekuwa Jeshi kubwa wakati wa uchaguzi tu jambo hili sio sawa Jeshi kubwa ni lile linalofanya kazi kubwa wakati wa Amani na kuongoza mapambano.
“Na sisi wakati wa kawaida ndio wakati wa kuimarika na kuhamasisha na kuusimamia na uhai ili wakati wa pambano Jeshi letu litusaidie.Mwakani kuanzia Februari tunaanza uchaguzi na hicho ndio kipimo cha kuona kwamba ninyi ni jeshi kubwa na maana nyingine,”amesema.
ASIKITISHWA NA MATENDO YAO
Amesema licha ya wanawake kuwa ni jeshi kubwa lakini baadhi wamekuwa wakifanya matendo ambayo sio mazuri.
“Wanawake ni Jeshi kubwa lakini baadhi yenu wanawaangusha Jeshi hili hasa kwa vitendo vyao na matendo yao na hivi karibuni tumeona mambo ya aibu yanafanyika ni maeneo mengi hayatujengei sura nzuri yanachafua sura yetu.
“Nikuhakikishie sisi ni wakali na tutaendelea kuwa wakali mtu yeyote akifikia kwamba anauwezo wa kufanya mambo yake ya hovyo na sisi tukamchekea na kumwangalia sio wakati huu.Ukiwa kiongozi lazima uwe unajiheshimu na unajua majukumu yako,”amesema.
WANAOJIPANGA
Katibu Mkuu huyo pia amesema wale wanaojipanga na kujipitisha kugombea nafasi mbalimbali wanatakiwa kuachwa kwani hakuna mahali panaporuhusu utaratibu huo mbovu.
“Mimi niwaombe mkisikia dalili watu wanaojipanga katika nafasi muwaache hata UWT hakuna mahali panaporuhusu utaratibu huu na utaratibu huu ni wa hovyo na hautusaidii kupata viongozi wazuri.
“Nimeona niliseme hilo kwa sababu moja ya sifa ya vikao vyetu mara nyingi hutumikia kupanga safu na hutumika kutengeneza makundi badala ya kutengeneza umoja hutumika kutengeneza miundombinu ya kujiwekaweka mahali fulani ili ukubalike badala ya kutengeneza miundombinu ya chama chetu kiheshimike,”amesema.
KWENDA KWENYE MASHINA
Amesema ndani ya chama wamefanya mapitio na kugundua wameteleza kwenye kusimamia misingi kuanzia ngazi ya shina.
Amesema wameanza kwenda katika mashina kuwahamasisha wananchi kwani ndiko wanakopatikana.