Viongozi wakikagua shamba la mapararachichi la mradi mdogo wa Eco Schools katika Shule ya Msingi Lulanda, wilayani Mufindi mkoani Iringa.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Msifuni wilayani Mvomero mkoani Morogoro wakiwa mbele ya shamba la migomba shule yao lilifadhiliwa na Program ya Eco Schools.
Na Suleiman Msuya
PROGRAM ya Eco Schools ilianza mwaka 1992 baada ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa (UN) wa Mazingira na Maendeleo ambao ulitambulika kama wa Rio de Janeiro Earth Sumitt.
Unatajwa kuwa ni moja ya mikutano mikubwa ya UN ambao ulifanyika kuanzia Juni 3 hadi 14 mwaka 1992.
Hii ni program ya kimataifa inayosimamiwa na Taasisi ya Elimu Duniani (Foundation for Enviromental Education (FEE) ambayo inahamasisha vijana wadogo kujihusisha na kulinda na kutunza mazingira endelevu.
Program hii inaanzia katika ngazi ya madarasa kwenye shule ambapo inatanuka hadi kwa jamii inayozunguka jamii hizo kwa ujumla.
Kupitia Program ya Eco Schools wanafunzi na vijana wanapata uzoefu wa kuona mafanikio ya kuzungumzia na kusimamia mazingira na sera ambapo wanapopata matokeo hutunikiwa bendera ya kijani.
Ofisa Elimu na Mazingira Msaidizi anayesimamia Program ya Eco Schools kutoka Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) Francis Fanuel, anasema program hiyo inatekelezwa na shule 59,000 dunia na zaidi ya wanafunzi milioni 17 wamejisajiliwa katika nchi 67.
Fanuel anasema TFCG inaamini katika elimu kwa maendeleo endelevu kwamba elimu itakayopatika isaidie mwanafunzi, leo, kesho na kesho kutwa kufikia ndoto zake.
Anasema Eco Schools imeweka muogozo wa kujifunza na kutenda ambao unatoa nafasi ya mafanikio kwa kuunganisha elimu endelevu katika mitaala ya kila siku ya shule ikiwa ni pamoja na kujenga ukaribu wa shule na jamii zinazowazunguka.
Ofisa huyo anasema Program Eco Schools inatekelezwa kuanzia shule za awali hadi vyuo vikuu lengo ni kuhakikisha Tanzania na dunia inakuwa na kizazi kinachotambua umuhimu wa utunzaji na uendelezaji mazingira.
“Hapa Tanzania Program ya Eco Schools ilianza na shule 20 kupitia TFCG mwaka 2016 katika vijiji vilivyopo wilayani Mvomero na kutanuka hadi Kilosa, Morogoro mkoani Morogoro na Mufindi mkoani Iringa ambapo awamu ya tatu iliisha mwaka 2020 ikihusisha shule 150 hadi 2023,” anasema.
Anasema program hiyo hapa nchini inasaidia shule za vijijini kutekeleza lengo la Eco Schools ambapo lengo kuu ni kuboresha maisha na kukuza uraia kupitia elimu kwa maendeleo endelevu.
‘Malengo mahususi ni pamoja na kujengea uwezo wa wasimamizi wa elimu katika ngazi zote ili waweze kupata rasilimali za utoaji wa elimu bora kwa maendeleo endelevu.
Kuongeza mtandao wa Eco-schools /kutanua wigo ili kufikia shule nyingi ziadi na kufanya uraghibishi ili elimu kwa maendeleo endelevu iwe kipaumbele kwenye sera na mipango ya taifa,” anasema Fanuel.
Aidha ametaja faida za Eco-school kuwa ni kuboresha mazingira ya shule, kuongeza rasilimali za shule hasa kipato ili shule iweze kupunguza changamoto zake ikiwemo utoaji wa chakula na uboreshaji wa miundombinu.
Pia kuwapa watoto stadi za maisha, kujengea uwezo walimu na kuwaongezea mbinu za kufundishia kwa kutumia mbinu shirikishi ili kuongeza ufaulu, kupunguza mdondoko na utoro shuleni.
“Uanzishwaji wa miradi shuleni ambapo shule huwa sehemu ya jamii kujifunza na kuanzisha miradi katika maeneo yao,” anasema.
Fanuel anasema tangu program hiyo ianze shule husika zimeweza kufanikiwa katika kuhifadhi mazingira, uendeshaji wa mazingira ya kujifunzia na kufundishia pamoja na utoaji chakula kwa wanafunzi.
Ofisa huyo anasema wanaamini shule ambazo zinatoa chakula kwa wanafunzi zinapata matokeo chanya mbeleni kwa kuongeza ufaulu.
Pia anasema Eco Schools tunasimamia dhana ya hatua saba ili kutekeleza program ambapo hatua ya kwanza ni kuunda kamati inayohusisha wajumbe wa shule na jamii.
“Upande wa shule wanatoka watu saba ambapo wanne ni wanafunzi na walimu watatu na upande wa jamii watu wanne kwa uwiano sawa.
Hatua ya pili ni kufanya tathmini shuleni ya mazingira, shuleni kuna nini, changamoto ni nini, imekaaje. Hatua ya tatu ni kutengeneza mpango kazi wa kutatua changamoto zilizopatikana,” anasema.
Fanuel anasema hatua ya nne ni kufanya ufuatiliaji je wapo kwenye mstari au wamepotea na hatua ya tano wanahusisha mtaala ili kuhakikisha wanachofundisha kwenye mazingira kinahusika na mtaala wenyewe mfano kuingiza jumbe za mazingira.
Anasema hatua ya sita ni kuhusisha jamii nzima kwenye masuala ya Eco Schools na mwisho ni kutengeneza jumbe mbalimbali za mazingira mfano shule ina changamoto ya mmomonyoko wa udongo, hivyo unaweza kukuta jumbe zimeandikwa tupande nyasi kuzuia mmomonyoko.
“Ukifanikiwa kutumiza hatua hizo saba shule inazawadiwa bendera ya kijani ambayo itakutambulisha kuwa umetmiza vigezo vya kimataifa,” anasema.
Fanuel amesema hadi sasa program ua Eco Schools imefanikiwa kufikia shule 97 katika wilaya hizo na maelengo yao ni ifikapo 2023 watakuwa wamefikia shule zaidi ya 150.
Anasema program hiyo imekuwa ikitoa mitaji kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali kama ya kilimo, mifugo na mingine ambayo inangiza kipato na kufundishia wanafunzi hasa kuwavutia wanafunzi wasiopenda kwenda shule.
“Zipo shule ambazo zinafuga samaki, nyuki, kulima migomba na mazao mengine jambo ambalo linazalisha wajasiriamali wengi kwa siku zijazo,” anasema.
Ofisa huyo anasema changamoto kubwa ambayo wanakutana nayo ni shule nyingi kuhitaji program hiyo ambayo imepata mwitikio mkubwa kwa jamii na shule husika.
Fanuel anasema Serikali inawajibu wa kuendeleza programa ya Eco Schools kwa sababu imeshaonesha matokeo chanya tangu kuanza kwake.
Halikadhali ameshauri wadau wengine kujitokeza na kuungana na TFCG ambao wameweza kusaidia watoto wengi wa Kitanzania kutunza mazingira kwa njia endelevu huku wakinufaika kiuchumi na kijasiriamali.
Ofisa Program wa Eco Schools Wilaya ya Mvomero, Judith Kiwale, anasema program hiyo inatekelezwa kwenye shule 97 ambapo lengo lao ni kupunguza changamoto ambazo zinakabili sekta ya elimu Tanzania.
Kilawe anasema TFCG kupitia mradi huo wa Eco Schools wanaamini wanafunzi takuwa mabalozi wazuri wa utunzaji mazingira lakini pia wanapata ujuzi wa kilimo, uhifadhi na elimu endelevu.
“Program hii imelenga kuboresha maisha na elimu kwa maendeleo endelevu ambapo tunashirikiana na serikali kuhakikisha hilo linatokea katika shule na vijiji husika,” anasema.
Anasema wamekuwa wakiwezesha shule kuandika miradi ili waweze kutunza mazingira na kuongeza kipato ili waweze kujikimu na kuhamasisha utunzaji mazingira kizazi hadi kizazi.
Naye Mzee Sokoyet anasema Serikali ya wilaya inatoa shukrani kwa wahifadhi ambao wamechochea utunzaji mazingira na maendeleo kwa shule zao.
Wakizungumzia mradi Eco Schools wanafunzi wa Shule ya Msingi Mkindo A na B wilayani Mvomero mkoani Morogoro wanasema mradi huo umechochea utunzaji wa mazingira na uhifadhi.
Wanasema wamejifunza kuanzisha vitalu ambapo wanaotesha miche na kuipanda kuzungusha shule na maeneo jirani.
“Mfano shule ya Msingi Mkindo B wamepanda miche 355 ya mbao, 235 ya matunda na 420 ya migomba jambo ambalo linanufaisha shule na wanafunzi,” anasema mwanafunzi mmoja.