Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo ,akizungumza na wanachama wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) Jijini Dar es Salaam uliofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).
Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo akiwa katika picha ya pamoja na wanachama wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) Jijini Dar es Salaam uliofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).
…………………………………………………………………………..
Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo amewataka wanachama wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) kujadili maendeleo ya viwanda zaidi kuliko changamoto zinazokabili viwanda nchini ambazo Serikali imeahidi kuzitatua.
Prof Mkumbo alisema hayo alipokutana na wanachama wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) Jijini Dar es Salaam uliofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).
Aidha aliwataka wanachama wa CTI kujadili ni jinsi gani wanaendeleza Viwanda nchini ikiwa ni pamoja na kuendeleza na kuwekeza katika maeneo yote ya Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) ambayo ni ajenda ya kitaifa.
Serikali inatambua mchango mkubwa wa mapato ya nchi unatokana na sekta binafsi hivyo inaweka mazingira wezeshi na rafiki kwa wawekezaji na itashirikiana na wadau kutatua changamoto zinazokabili viwanda nchini ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi kwenye biashara. Alisema Prof. Mkumbo.
Prof. Mkumbo, aliahidi kutoa ushirikiano kwa sekta binafsi ili kujenga mazingira bora na kuaminiana baina ya Serikali na sekta binafsi.
“Serikali haina mpango wa kukwamisha sekta binafsi bali itaendelea kuwawekea mazingira mazuri na bora ya kufanyia biashara,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa CTI, Paul Makanza alisema katika mkutano huo walijadili kuhusu hali ya viwanda nchini ikiwa ni pamoja na kuonyesha changamoto wanazokabiliana nazo na jinsi ya kuzitatua.
“Tumejadili ni namna gani tunaweza kuongeza tija katika uzalishaji, namna gani tunaweza kutatua tatizo la ujuzi, ni mapendekezo gani tunaweza kupeleka kwa serikali ili kuhakikisha mazingira ya biashara yanaweza kuwa mazuri,” alisema.
Kwa upande wake mdau wa viwanda, Shabbir Khataw alisema amefurahi kwa kuwa Serikali imeahidi kuwa pamoja nao kwani inatambua mchango mkubwa wa mapato ya nchi yanatokana na sekta binafsi.
Veronika Mbazingwa kutoka kiwanda cha Chemi Cotex alisema baada ya Waziri Mkumbo kuzungumza nao ni dhahiri kuwa Serikali ipo tayari kushirikiana nao katika changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.
“Hii inatupa mwanga kwamba kwenye viwanda kutakuwa na mazingira ambayo yatasaidia katika ushindani wa bidhaa zetu katika masoko ya ndani hata nje ya nchi.
“Kwa upande wa viwanda tunaona kuna haja ya Serikali kuangalia upande wa nguvu kazi inayotumika kiwandani tungependa kuona ni namna gani ambavyo tunapata wafanyakazi wenye ujuzi tuwe na malengo madhubuti ya kupata watu wanaoweza kusimamia viwanda, tunaongelea wale wahandisi watakaoenda kwenye mashine na kufanya kazi,” alisema.
Alisema anaamini miaka mitano ijayo watakuwa wamepata nguvu itakayoleta ushindani mkubwa katika viwanda vyao.
“Tunaamini mazingira wezeshi, mazingira mazuri ya biashara yataendelea kuboreshwa,” alisema.
Tanzania imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda, imepiga hatua miaka mitano iliyopita hivyo inatarajia kuendeleza kasi hiyo katika miaka mingine mitano.