Mkutano wa 14 Baraza la
Kisekta la Mawaziri wa Kilimo na Usalama wa Chakula wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki kwa Ngazi ya Makatibu Wakuu umefanyika hivi karibuni jijini
Arusha ikiwa ni maandalizi ya mwisho kuelekea Mkutano wa Mawaziri utakaofanyika
jijini hapa tarehe 25 Juni 2021.
Lengo la Mkutano wa 14 wa
Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Kilimo
na Usalama wa Chakula pamoja na mambo mengine ni kupitia na kujadili
utekelezaji wa maamuzi na maelekezo ya Baraza la Mawaziri wa Jumuiya pamoja na
kupitia na kujadili masuala mbalimbali
muhimu ya kisera, kimkakati, miradi na program zinazotekelezwa katika
sekta ya kilimo.
Katika Mkutano wao, Makatibu
Wakuu, pamoja na mambo mengine wamepokea na kupjadili agenda mbalimbali
zilizowasilishwa kwao na Wataalam ikiwemo, Taarifa ya Usalama wa Chakula ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki; Taarifa kuhusu Mradi wa Afrika wa Kilimo cha
Ushindani cha Mpunga kwa Kanda ya Afrika Mashariki; Taarifa kuhusu Maendeleo ya
Mifugo; Taarifa kuhusu Mradi wa Kuzuia na Kudhibiti Sumukuvu; Taarifa kuhusu
Maendeleo ya Uvuvi; na Taarifa kuhusu Uhamasishaji wa Uchangiaji Rasilimali.
Awali akifungua Mkutano huo, Mwenyekiti
ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Ushirika wa Kenya,
Prof. Hamadi Iddi Boga ametoa rai kwa wajumbe wa mkutano huo kuendelea
kushirikiana katika kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta
ya kilimo kwenye jumuiya ili
kujihakikishia usalama wa chakula.
Amesema kuwa changamoto nyingi
za kilimo zinazozikabili nchi wanachama
zinafanana hivyo ni vizuri nchi zote zikajikita kufanyia kazi changamoto
hizo pamoja na kutekeleza program na maazimio yanayofikiwa kwenye mikutano
mbalimbali ili hatimaye kuboresha sekta ya kilimo na usalama wa chakula ambayo
ni muhimu kwa ustawi wa wananchi.
“Nawashukuru sana kwa kuja na
kushiriki kwenye mkutano huu muhimu. Naelewa kwamba usalama wa chakula ni jukumu
letu sote kama nchi wanachama na kwa vile tunapitia changamoto zinazofanana
ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na corona ni vizuri tukaja na mbinu za pamoja
kuzikabili changamoto hizo na kuendeleza sekta hii muhimu ya kilimo” alisema
Prof. Boga.
Katika hotuba yake
ililiyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Sekta za Uzalishaji katika
Sekretarieti, Bw. Jean Havugimana, Naibu
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughilikia Sekta za Uzalishaji
na Jamii, Mhe. Christophe Bazivamo amewashauri wafanyabiashara wa mazao ya
kilimo katika Nchi Wanachama kushirikiana na mamlaka zinazosimamia usalama wa
chakula na viwango ili kupata ushauri wa kitaalam kwa ajili ya kuzalisha bidhaa
salama na zenye ushindani katika soko. Kadhalika ameshauri elimu kuhusu kilimo
itiliwe mkazo kwa nchi wanachama ili kuzalisha wataalam wengi kwenye sekta hii
na pia kukuza ajira kwa vijana ambao ni kundi kubwa zaidi katika nchi
wanachama.
Kwa upande wake, mwenyeji wa
Mkutano huo ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo wa Tanzania, Dkt. Andrew
Massawe amewakaribisha na kuwashukuru wajumbe waliosafiri kutoka kwenye nchi
zao hadi jijini Arusha licha ya changamoto ya ugonjwa wa Corona na kuwatakia mkutano mwema na wenye manufaa
kwa wananchi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano
wa Ngazi ya Makatibu Wakuu umeongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw.
Andrew Massawe na kuhudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid
Tamatama pamoja na Maafisa Waandamizi kutoka Sekta mbalimbali
zinazojishughulisha na masuala ya kilimo na usalama wa chakula hapa nchini.
Sehemu ya ujumbe wa Kenya ukishiriki Mkutano wa Makatibu Wakuu |
Kiongozi wa ujumbe wa Burundi kama anavyoonekana puchani |
Sehemu ya ujumbe wa sekretarieti katika mkutano |
Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania wakishiriki mkutano wa Makatibu Wakuu wanaoshughulikia sekt aya kilimo na usalama wa chakula |
Ujumbe wa Tanzania wakiwa kwenye mkutano |
Mkutano ukiendelea |
Wajumbe wakifuatilia matukio mbalimbli kwenye Mkutano |
Wajumbe kutoka Sekta za kilimo na usalama wa chakula wakishiriki Mkutano wa Makatibu Wakuu |
Mkutano ukiendelea |
Wadau wa kilimo wakiwa kwenye mkutano |
Mkutano ukiendelea |