……………………………………………………………….
Na Gift Thadey, Babati
MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Peter Sulle amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mikoa (ALAT) Mkoa wa Manyara.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, John Noya ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi huo, amemtangaza Sullle kushinda nafasi hiyo katika uchaguzi uliofanyika jana mjini Babati.
Noya amesema Sulle alishinda nafasi hiyo kwa kupata kura 11, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbulu Joseph Mandoo alipata kura nane na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ Rose Kamili kura nane.
Amesema Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga Laizer alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Manyara kwa kupata kura zote 27 baada ya kukosa mpinzani.
Sulle akizungumza baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Manyara, aliwashukuru wajumbe wote kwa imani kubwa waliyonayo kwake na kumchagua kushika nafasi hiyo.
Laizer amewashukuru wajumbe kwa kumpa kura zote 27 na akaomba ushirikiano kwa lengo la maslahi mapana ya Manyara nzima na siyo kunufaisha halmashauri moja pekee.
Diwani wa viti maalum wa Tarafa ya Naberera Wilayani Simanjiro, Bahati Partison amechaguliwa kuwa mjumbe wa kundi la wanawake ALAT Taifa kutokea Mkoa wa Manyara kwa kupata kura 12, baada ya kuwashinda Zainab Sige wa Halmashauri ya Mji wa Babati kwa kura nane na Flaviana Maasay wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, kwa kura saba.
Madiwani wawili, Isabela Gabriel wa viti maalum Tarafa ya Endasak wilayani Hanang’ na diwani wa Kata ya Qash wilayani Babati, Idd Gitianga walichaguliwa kuwa wajumbe wa kamati tendaji ALAT Mkoa wa Manyara.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, John John Nchimbi ameteuliwa na Wajumbe wa ALAT Mkoa wa Manyara, kuwa Katibu Mtendaji wa ALAT Mkoa wa Manyara.
Mweka hazina wa halmashauri ya wilaya ya Babati, Frank Kasabele ameteuliwa kuwa mhasibu wa ALAT wa mkoa wa Manyara.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Tamim Kambona waliteuliwa kuwa wajumbe wa kamati tendaji ALAT Mkoa wa Manyara