Watoto wakikabidhiwa miche ya matunda
*************************
Na. Zillipa Joseph, Katavi
Katibu Tawala wa wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi Geofrey Mwashitete ameitaka jamii kujenga mazoea ya kuwahusisha watoto katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo utunzaji wa mazingira hali itakayopelekea manufaa makubwa kwa nchi kwa nyakati za sasa na zijazo
Mwashitete ametoa kauli hiyo katika kilele cha wiki ya mazingira wilaya iliyofanyika katika shule ya msingi Kapemba kata ya Mishamo wilayani humo
Alisema sehemu mojawapo ya kufikisha ujumbe kwa jamii nzima ni kuhusisha watoto hasa wenye umri mdogo kwani wao wanashika sana wanachoambiwa
“Hawa watoto ukiwaambia wanabeba hivyo hivyo lilivyo, sio watu wazima wana mambo kibao kichwani, kwa hiyo hawa watoto wakihusishwa ipasavyo hakika kutakuwa na mabadiliko chanya siku zijazo’ alisema Mwashitete
Mwashitete amekabidhi miche 3,000 ya miti ya matunda kwa watoto hao ili ikapandwe katika mazingira wanayoishi
Bwana Paulo Mjema ni Afisa kutoka katikaTaasisi ya Janegoodall inayojihusisha na masuala ya utunzaji wa misitu katika mikoa ya Katavi na Kigoma, amesema mbali na kutoa miche hiyo pia wameanzisha klabu za mazingira za watoto ili kuleta mwamko kwa jamii
Mjema amesema klabu hizo zinafundishwa mambo mbalimbali ya utunzaji wa mazingira ambapo pia wamewagawia mizinga ya kisasa ya kufugia nyuki
Mizinga hii itawapa faida kwani ni familia nzima itafaidika na mazao ya nyuki, tunaamini na miche ya miti ya matunda tuliyotoa itasaidia kuibadilisha jamii dhidi ya uharibifu wa mazingira
Hata hivyo hatutaishia hapo klabu hizi tutazifikisha mpaka darasa la pili na la tatu na kuwaanzishia bustani za miti ambazo zitakuwa zikisimamiwa na walimu wao
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii wilaya hiyo Bi. Halima Haidary amesema watoto wadogo wana mchango mkubwa katika kufanikisha mabadiliko ya tabia ya wanajamii
‘Unajua watoto ni kama vitabu, neno likimuingia sawasawa kichwani halitoki, watoto wakipata mafunzo na ikafanywa kuwa endelevu kwanza tayari utakuwa umewafundisha kuandaa vitalu vya miti ambayo baadae akiwa mtu mzima anaweza kuitumia kama ajira yake badala ya kwenda kuchoma mkaa na akawa balozi mzuri tu wa upandaji miti’ alisema Halima