Mkuu wa kitengo cha Uhusiano na Masoko (TBS) Bi.Gladness Kaseka akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) leo Jijini Dar es Salaam.
**********
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wafanyabiashara na wajasiriamali nchini kujitokeza katika Maonesho ya biashara ya kimataifa ya 45 Sabasaba yanayotarajiwa kuanza Juni 28 katika Viwanja vya Maonesho vya Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo katika Ofisi za TBS Jijini Dar es Salaam Mkuu wa kitengo cha Uhusiano na Masoko (TBS) Bi.Gladness Kaseka amesema kuwa kutakuwa na huduma ambazo watakuwa wanatoa papo hapo kulinganisha na maonesho ya kipindi kilichopita kama huduma ya usajili wa majengo ya bidhaa za chakula na vipodozi vitatolewa papo hapo
“Tutawapa msaada wa kujisajili kwenye mfumo ambapo ilikuwa ni changamoto ambayo wamepitia kwa muda mrefu tutawasaidia kujisajili kwenye mfumo pia tutawapatia mkaguzi palepale na kuweza kwenda kukagua mazingira yao ya biashara na kuwapatia kile kibari ndani ya siku moja”. Amesema Bi.Gladness.
Aidha Bi.Gladness amesema kipindi chote hicho cha Maonesho wafanyabiashara wanaopeleka biashara na bidhaa nje ya nchi watapata huduma na taarifa mbalimbali za masoko ya bidhaa zao ili kuepuka vikwazo vya biashara wanapokua wakifanya biashara nje ya nchi.
Pamoja na hayo Bi.Gladness amewataka wale ambao wanahitaji huduma za viwango kufika katika maonesho hayo kwasababu kutakuwa na huduma za kuuza viwango katika banda lao pia watatoa elimu kwa wadau mbalimbali wa viwango.