Shehe wa mkoa wa Arusha , Shaaban Juma akizungumzia kuhusiana na kuwepo kwa wimbi hilo la ombaomba wanaovalia nguo za kiislamu jijini Arusha,
………………………………………………………………
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha.Shehe wa mkoa wa Arusha, Shabaan Juma ametoa onyo kali kwa waumini wa dini ya kiislamu mkoani Arusha ambao wamekuwa wakiwatumia watoto kuomba fedha kwa watu kitendo ambacho ni kinyume na maadili ya dini hiyo,hivyo kuacha mara moja tabia hiyo.
Aliyasema hayo wakati akizungumza na mwananchi ofisini kwake kuhusiana na tabia hiyo ambayo imekuwa kero kwa jiji la Arusha.
Alisema kuwa,kumekuwepo na baadhi ya waumini wa dini hiyo ya kiislamu wamekuwa wakitumia watoto wadogo kuomba mtaani huku wakiwa wamevalia mavazi ya kiislamu ,jambo ambalo alisema kinadhalilisha dini hiyo ya kiislamu.
Alifafanua kuwa,jambo hilo yeye mwenyewe ameliona katika maeneo mbalimbali jijini hapa,ambapo aliwataka kutafuta njia mbadala ya kujipatia kipato badala ya kuomba kwani maadili ya dini hiyo yanakataza kufanya hivyo.
“kwa kweli watoto hawa ni wengi Sana hasa hapa katikati ya mji na wakati mwingine kuna wanawake wamekuwa wakikodisha watoto wachanga na kuzunguka nao huku wakidai kuwa wao ni wajane na kuwa wanaishi mazingira magumu ,Jambo ambalo wengi wao ya wamekuwa wakidanganya ni namna tu ya kujipatia kipato,kwa kweli naomba Sana hao wanaofanya hivyo waache mara moja watafute kazi za kufanya kwani haipendezi kwa muumini wa dini ya kiislamu kufanya hivyo.”alisema Shehe .
Aidha alisema kuwa, kutokana na swala hilo wao Kama uongozi wa mkoa wamejipanga kuwaita watu hao na kukaa nao pamoja na wadu mbalimbali ili waweze kuona namna ya kuwasaidia na kuweza kusaidia ili waweze kufanya shughuli mbalimbali na kuweza kujipatia kipato na kuondokana na kazi hiyo.
Nao baadhi ya watoto hao ambao wamekuwa wakiombaomba katikati ya mji,Aisha Bakari na Mwajuma Mohamed wakazi wa eneo la Ngarenaro mjini hapa,walisema kuwa, wao wamekuwa wakitumwa na wazazi wao kufanya hivyo kwani wengi wao wametelekezwa na baba zao na kuwa wanaishi mazingira magumu Sana.
“Mimi nimekuwa nikiishi na mama yangu kwa muda mrefu baada ya baba yetu kuondoka na kutuacha tukiwa wadogo wakati ndo tulikuwa tunamtegemea yeye,Sasa nina wadogo zangu watatu unategemea tutakula nini mama yangu na yet anaombaomba na Mimi huku naomba ili mwisho wa siku tupate riziki ya wadogo zangu na hata kulipia kodi sio kwamba tunapenda kufanya hivyo.”alisema Aisha.
Mmoja wa mwanamke ambaye huomba na mtoto mchanga,Amina Rashidi alisema kuwa,yeye ana watoto watatu ambapo baada ya kupata watoto hao mwanaume alimtelekeza miaka mitatu Sasa imepita na kuondoka kutokana na hali ngumu ya maisha na kuwa hajui alipo hadi Sasa hivi na hana msaada mwingine wowote wa kujipatia kipato ili alishe watoto wake .
Aidha waliomba wadau mbalimbali watakaoweza kuwasaidia wapo tayari kusaidiwa ili waondokane na shughuli hiyo ya kuomba kwani hata wao wenyewe hawapendi inawalazimu kufanya hivyo ili wapate riziki.
Hata hivyo swala hilo la watu kuomba kuomba katika jiji la Arusha limekuwa changamoto kubwa Sana huku wazazi wakiwatumia watoto wadogo kwenda kuombaomba na kufuata watu kwenye magari ili waweze kupatiwa riziki,ambapo juhudi zaidi zinatakiwa kwa wadau mbalimbali kuweza kuwasaidia na kuweza kujishughulisha na shughuli nyingine za kujipatia kipato.