**************************
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MKUU wa mkoa wa Pwani ,Aboubakar Kunenge amewaapisha wakuu wapya wa wilaya ambao waliteuliwa hivi karibuni na Rais Samia Suluhu Hassan ambapo amewapa kazi ya kukabiliana na changamoto ya masuala ya migogoro ya ardhi kwenye wilaya zao.
Wakuu hao wa wilaya ya Kibiti, Mkuranga na Kisarawe wameapishwa mjini Kibaha sherehe ambazo zilifanyika kwenye viwanja vya ofisi ya mkuu wa mkoa na kuhudhuriwa na watu wakiwemo watumishi na ndugu wa wakuu hao wapya wa wilaya.
Kunenge alieleza,wakuu hao wa wilaya wanapaswa kuwasikiliza wananchi ili kutatua kero zinazowakabili na kama kila mtendaji kuanzia ngazi za chini itasaidia kutatua kero zinazowakabili wananchi na hakuna kiongozi mmoja kutatua kero zote za wananchi lazima washirikiane.
“Tatueni kero na kuondoa migogoro na kuongeza vyanzo vya mapato kwani bila ya mapato serikali haiwezi kuleta maendeleo na miradi ikamilike kwa wakati na kwa thamani ya fedha,”alisema Kunenge.
Alisema kuwa moja ya mambo ambayo yanakwamisha mkoa wa Pwani ni ardhi ni tatizo kubwa kwani baadhi hata wawekezaji wameshindwa kuendelea na shughuli na wahakikishe watu hawaonewi.
Aidha aliwataka wakuu hao wa wilaya kujenga mahusiano mazuri na chama na wasione kama kero pale wanapotakiwa kutoa taarifa mbalimbali za utekelezaji wa ilani ya CCM.
Mkuu wa wilaya ya Mkuranga Hadija Nasir Ali alieleza atahakikisha anasimamia sheria na utaratibu ili kutatua changamoto ili watu waweze kuishi kwenye mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao bila ya tatizo lolote.
Kwa upande mkuu wa wilaya ya Kibiti Kanali Ahmed Abas alisema kuwa atahakikisha uzalishaji mali unakuwa juu pamoja na kuhakikisha makusanyo ya Halmashauri yanakuwa juu ili kuharakisha maendeleo.
Mkuu wa wilaya ya Kisarawe Nickson Simon “Nick wa Pili” alisema kuwa moja ni kutatua kero za wananchi ambazo wamepewa maelekezo na mkuu wa mkoa ikiwa ni pamoja na kutatua kero za wananchi na kubwa ni utatuzi wa migogoro ya ardhi ambayo imekithiri.
Simon alisema kuwa wataanza kutekeleza vipaumbele vya mkoa na atatumia vipaji na uwezo na mawazo yake ili kuleta maendeleo kwa kuleta mambo mapya ya kimaendeleo.
Naye mkuu wa wilaya ya Kibaha ambaye amehamishiwa Kibaha kutokea wilaya ya Kigamboni Ruth Msafiri alisema kuwa atashirikiana na wananchi wa Kibaha katika kutatua changamoto zao.
Hivi karibuni Rais aliteuwa wakuu wapya wa wilaya na kuwahamisha wale wa zamani kwenda maeneo mengine ambapo kwa wakuu wa wilaya aliohamihia mkoani Pwani ni pamoja na Kapteni Gowelle ambaye anakuwa mkuu wa wilaya ya Rufiji na Mhandisi Martin Ntemo ambaye amehamishiwa wilaya ya Mafia akitokea Kibaha na Zainab Issa ambaye anakuwa mkuu wa wilaya ya Bagamoyo.