Home Michezo MBUNGE CUP YAPAMBA MOTO WILAYANI LUDEWA

MBUNGE CUP YAPAMBA MOTO WILAYANI LUDEWA

0

……………………………………………………

Na Damian Kunambi, Njombe.

Mashindano ya ligi ya mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga yameendelea kushika kasi Katika kata mbalimbali wilayani Ludewa mkoani Njombe ambapo kwa sasa yapo katika hatua ya makundi kwa ngazi za vijiji.

Mashindano hayo ambayo yalizinduliwa  hivi karibu na kuhusisha kata zote 26 za wilaya hiyo ambapo katika kila kata  atatoka mshindi na kushindanishwa katika ngazi ya tarafa kisha wilaya.

Akizungumzia mashindano hayo mbunge huyo amesema kuwa katika kufanikisha mashindano hayo ametoa jezi seti 140 pamoja na mipira 140 vyenye thamani ya shilingi Milioni 28.

Amesema mashindano hayo yatakapo kamilika Katika ngazi ya kata timu itakayoibuka mshindi itajinyakulia kitita cha shilingi laki moja pamoja na kombe litakaloandikwa jina la kata huku mshindi wa pili akijinyakulia shilingi elfu hamsini.

“Mashindano haya ni endelevu ambapo yatakuwa yakifanyika kila mwaka na watakuwa wakishindania vikombe hivi ambavyo vinatolewa katika kila kata huku katika ngazi ya tarafa na wilaya zikishindaniwa zawadi nyingine zaidi”. Alisema Kamonga.

Ameongeza kuwa timu zitakazoshinda kwa ngazi ya tarafa na wilaya zitapewa zawadi kubwa zaidi kuliko zilizotolewa kwa washindi wa ngazi ya kata.

Aidha kwa upande wa mmoja wa wasimamizi wa mashindano hayo kutoka Katika chama cha mpira wa miguu wilayani humo Jimmy Haule amesema mashindano hayo yameanza vyema ambapo tayari kuna timu 123 kutoka katika vijiji vyote 77 vya wilaya hiyo ambazo zinashiriki mashindano hayo.

Amesema kila kata tayari mashindano hayo yanaendelea na wamekuwa wakifanya mawasiliano na wasimamizi wa mashindano katika kata zote ili kuona endapo kuna changamoto zozote zinazojitokeza.

“Tumekuwa tukiwasiliana na wenzetu wanaoongoza mashindano katika kila kata lakini changamoto kubwa inakuja ni jinsi ya kuyafikia maeneo hayo endapo kunatokea changamoto kutokana na jografia ya wilaya yetu pamoja na miundombinu isiyo rafiki kwa kufika huko inapelekea kutofika kwa wakati hivyo tunalazimika kuahirisha mechi mpaka tutakapotatua changamoto hiyo”, Alisema Haule.

Nao washiriki wa mashindano hayo wamempongeza mbunge huyo kwa kuwaandalia mashindano hayo kwani kwa kufanya hivyo yanaleta ushirikiano mzuri baina yao sambamba na kujenga afya zao huku wakijiepusha na kujihusisha na vitendo vya uhalifu.

Gabriel Gama ni mmoja wa washiriki hao amesema mbunge huyo amejitoa sana katika kuwasapoti hivyo amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza kumuunga mkono mbunge huyo.