Home Mchanganyiko NKWAMA: TUSISUBIRI WALIMU WATENDE MAKOSA ILI TUWAADHIBU

NKWAMA: TUSISUBIRI WALIMU WATENDE MAKOSA ILI TUWAADHIBU

0

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Paulina Nkwama (kushoto) akiongea na watumishi wa TSC Wilaya ya Dodoma alipofanya ziara ofisini hapo hivi karibuni. Pembeni yake ni Kaimu Katibu Msaidizi wa TSC Wilaya ya Dodoma, Leticia Mwakasitu.

Kaimu Katibu Msaidizi wa TSC Wilaya ya Dodoma, Leticia Mwakasitu (kulia) akitoa ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa majukumu ya ofisi yake kwa Katibu wa TSC, Paulina Nkwama.

Baadhi ya Watumishi wa TSC Wilaya ya Dodoma wakisikiliza maelekezo ya kiutendaji kutoka kwa Katibu wa TSC, Paulina Nkwama (hayupo pichani) wakati wa ziara ya Katibu huyo katika ofisi za TSC Dodoma. Pichani, anayeandika ni Afisa anayeshughulikia Nidhamu na Maadili ya Walimu kutoka TSC Makau Makuu, Julius Mshana.

Katibu wa TSC, Paulina Nkwama akiasini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili ofisi za TSC Chamwino kwa ziara ya kikazi iliyofanyika hivi karibuni.

Katibu wa TSC, Paulina Nkwama (Kulia) akipitia orodha ya Walimu waliopanda Madaraja katika Wilaya ya Chamwino wakati wa ziara yake katika ofisi za TSC wilayani hapo aliyoifanya hivi karibuni. Pichani, upande wa kushoto ni Kaimu Katibu Msaidizi wa TSC Wilaya ya Chamwino, Paulina Kanumba na katikati ni Afisa Ajira na Maendeleo ya Walimu wa ofisi hiyo, Pater Nassa.

…………………………………………………………………….

Na Adili Mhina.

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Paulina Nkwama amewataka watendaji wa Tume hiyo kujikita zaidi katika kutoa elimu kwa walimu ili wazingatie maadili ya kazi yao badala ya kukaa na kusubiri watende makosa ili wawachukulie hatua za kinidhamu.

Agizo hilo amelitoa hivi karibuni alipofanya ziara katika ofisi za TSC Wilaya ya Dodoma na Chamwino kwa lengo la kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa majukumu ya kila siku pamoja na kuona namna ofisi hizo zinavyotoa huduma kwa wateja katika wiki ya Utumishi wa Umma.

Nkwama alisema kuwa TSC ina wajibu wa kuwasaidia walimu katika masuala ya maadili na maendeleo ya utumishi wao ili wawe na ustawi mzuri na kufanya watoe elimu bora kwa wanafunzi.

“Tumepewa dhamana ya kuwahudumia walimu katika masuala ya ajira, maadili na maendeleo yao. Sasa ni lazima tujikite katika kuzuia walimu wasijiingize katika vitendo vya uvunjifu wa maadili kwa kuwa wakiwa na maadili mema ndipo tunaweza kujivunia kuwa tunafanya kazi,” alisema.

Aliwataka watendaji wa ofisi hizo kuhakikisha wanatumia muda wao kuwafikia walimu na kuwapa elimu kuhusu haki, wajibu na maadili ya utumishi ili kuwaepusha na makosa ya kinidhamu.

Aliongeza kuwa mamlaka za nidhamu ambazo ni wakuu wa shule na TSC ngazi ya wilaya hawajatekeleza wajibu wao ipasavyo katika kuwasaidia walimu kuelewa umuhimu wa kuzingatia miiko na maadili ya kazi yao katika utendaji wa kazi.

Alifafanua kuwa mamlaka hizo zinapaswa kubaini mienendo ya walimu isiyofaa na kuwarekebisha mapema kabla ya kufikia hatua ya kuanzisha shauri la nidhamu ambao linaweza kusababisha mwalimu apoteze ajira yake.

“Haiwezekani mkuu wa shule anaona mwalimu siku ya kwanza hayupo shuleni, siku ya pili hayupo halafu badala ya kufanya jitihada za kumtafuta ili ajue tatizo na kuona namna ya kumsaidia, anasubiri siku tano ziishe apeleke taarifa kwa mkurugenzi ili hatua za kinidhamu zichukuliwe, hii siyo sawa,” alisema.

Aliongeza kuwa pale inapotokea mwalimu anafukuzwa kazi ni lazima mamlaka za nidhamu zijitafakari kama zinatekeleza wajibu wao wa kuwaelimisha walimu inavyotakiwa.

“Hatuwezi kujivunia kuwa tumefanya kazi nzuri endapo tunaona bado walimu wanafukuzwa kazi kwa makosa ya kinidhamu. Pale inapotokea tumemfukuza kazi mwalimu lazima tujiulize kuwa tumetekeleza wajibu wetu wa kutoa elimu na kumrekebisha mwalimu kama ianvyotakiwa,” alisisitiza.

Pamoja na kusisitiza hayo, Katibu huyo alisema pale ambapo mwalimu amerekebishwa lakini hataki kubadilika ni lazima mamlaka za nidhamu zimchukulie hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu husika.

Katika kuadhimisha wiki ya utumishi wa Umma, Katibu huyo alipata fursa ya kuona namna ofisi hizo zinavyopokea wateja na kuwahudumia, pia alipokea malalamiko na changamoto za watumishi wa ofisi hizo na kuahidi kuzifanyia kazi haraka iwezekanavyo ili waendelee kuwa na mazingira mazuri ya kufanyia kazi ya kuwahudumia walimu.