Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda amempa siku 7 Mrajisi wa vyama vya ushirika nchini, Dkt.Benson Ndiege kuhakikisha anaurejesha umoja wa vyama vya msingi 32 vya wakulima wa Kahawa (G32 KNCI JVE) vinavyofanya biashara ya kahawa nchini.
Waziri Mkenda ametoa agizo hilo kufuatia hatua ya Mrajisi wa vyama hivyo vya ushirika kuufuta umoja huo Agosti mwaka jana kwa madai ya kuwa biashara ya kahawa inapaswa kufanywa na chama cha ushirika KNCU pekee jambo ambalo amesema sio sahihi.
Akizungumza juzi katika mkutano wa 11 wa wadau wa Kahawa uliofanyika Jijini Dodoma ambao uliwakutanisha wakuu wa mikoa, wakuu wa Wilaya wakurugenzi, Taasisi za fedha pamoja na viongozi mbalimbali wa vyama vya msingi alisema endapo akishindwa kuurejesha umoja huo hatua kali zitachukuliwa dhidi yake ikiwemo kufutwa kazi.
“Kuna watu walikuwa wameungana wanajiita G32, nimempa Mrajisi wiki moja amalizane na hawa watu ili biashara ya kahawa iendelee, Kahawa ndio iliyotuletea ushirika wa kwanza hapa Tanzania na KNCU ilizaliwa kutokana na Kahawa na mimi sitaki ife ,”alisema Mkenda
“Ndani ya wiki hiyo moja nataka G32 iwe imeanza kazi kwasababu Kazi ya ofisi ya Mrajisi inatakiwa iwe facilitative maana kuna wengine walikuwa wanazuia Kahawa isiende kwenye uchakataji ,”alisema Profesa Mkenda
Akizungumza mara baada ya waziri kutoa agizo hilo, Meneja Mradi wa G32, Gabriel Ulomi aliishukuru serikali kwa maamuzi hayo na kusema kuwa ni moja ya hatua ya kuwarejeshea uhai.
“Kwa niaba ya kundi la vyama vya G32 tunashukuru awamu ya sita kusikiliza kilio cha wakulima wa Kahawa ambao tumekuwa tukikusanya Kahawa kutoka kwa wakulima na kuuza ndani na nje ya nchi kwa kurejeshea haki yetu ya kimsingi ya kufanya biashara kwa sheria za nchi kwa sababu ushirika ni uhai,”alisema Ulomi
“Sisi tulikuwa tukilazishwa na Mrajisi kurudi kwenye ushirika ambao una matatizo ambayo matatizo haya yaliyotokea G32 ikaanza yalikuwa hayajarekebishwa, tunamshukuru Waziri amesikiliza hilo na kuturudishia uhai wetu na hatutamwangusha ,”alisema Ulomi